Maofisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wamemkamata mshukiwa mkuu wa mauaji ya mtu aliyepigwa risasi katika tukio la ujambazi lililotokea kwenye duka la kutoa huduma za mtandao mjini Siaya mnamo Agosti 1, 2023.
Uchunguzi uliofanywa ulibaini kuna kundi la wahalifu linalojulikana kwa jina la ‘comrades’ na ambalo limehusika katika msururu wa wizi katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na ule wa Agosti 1.
DCI ilisema kwamba uchunguzi uliofuatia tukio la mauaji huko Siaya ulitambua mshukiwa Charles Otieno Odhiambo alihusika na matukio kadhaa ya unyang’anyi.
Kufuatia uchunguzi huo, polisi walianza kumsaka na akakamatwa Jumanne katika eneo la Awelo, Siaya.
Bidhaa na vifaa kadhaa ikiwa ni pamoja na nambari za usajili za pikipiki za KMGE 652Q na KMFM 231D, aina mbalimbali za simu na vifaa vya nyumbani, vitambulisho vya taifa, panga mbili zilipatikana katika nyumba yake.
“Mshukiwa amekuwa akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Yala akisubiri kufikishwa mahakamani, huku wapelelezi wakiimarisha msako wa washirika wake,” DCI ilisema katika taarifa.