RAIS wa Malawi, Peter Mutharika amewata wafuasi wake kupuuza matokeo yanayoripotiwa kwenye vyombo vya habari ambayo yanaonyesha mpinzani wake mkuu Lazarus Chakwera anaongoza.
Pamoja na kwamba Tume ya Uchaguzi ya Malawi MEC bado haijatangaza matokeo ya uchaguzi wa urais uliorudiwa , ishara za mapema zinaonesha kwamba Rais Peter Mutharika yuko nyuma ya Chakwera.
Kulingana na mgombea mwenza Atupele Muluzi, ambaye alisema kwamba ametumwa na Mutharika kuzungumza na vyombo vya habari, rais amewataka wafuasi wake kupuuza ripoti zinazosema ameshindwa katika uchaguzi huo, akisema wanapaswa kusubiri matokeo rasmi ya Tume ya Uchaguzi ya (MEC).
Atupele Muluzi ni mtoto wa rais wa zamani nchini humo, Bakili Muluzi na kiongozi wa chama kidogo cha upinzani United Democratic Party DPP.
Muluzi amedai kwamba takribani wachunguzi 15 waliotumiwa na DPP/UDP katika maeneo ya upinzani wametoweka na wengine kuhofiwa kufariki baada ya kushambuliwa na wafuasi wa upinzani.
Matokeo ya wilaya zote 28, yaliotiwa saini na maofisa pamoja na wawakilishi wa wilaya yanaonesha kwamba Rais Mutharika yuko nyuma ya Lazarus Chakwera ambaye anaongoza chama cha upinzani cha Malawi Congress na kinawakilisha muungano wa Tonse unaoshirikisha vyama vinane vya upinzani.
Juzi chombo cha habari cha serikali kiliripoti kuwa mgombea wa upinzani Chakwera anaongoza dhidi ya Mutharika.
Upinzani nchini Malawi unaelekea kupata ushindi katika kura ya uchaguzi wa urais wa marudio baada ya matokeo yake kufutiliwa mbali kutokana na madai mengi ya udanganyifu.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumanne hayajatangazwa na tume ya uchaguzi ya Malawi imesema itatangaza siku chache zijazo.
Lakini chombo cha habari cha serikali MBC kinasema kwamba kiongozi wa upinzani, Chakwera alikuwa anaongoza na asilimia 59 ya kura zilizohesabiwa siku ya Jumatano.
Kilisema Rais Peter Mutharika , ambaye anawania muhula wa pili ana asilimia 38 ya kura zilizohesabiwa.
Mgombea wa tatu ambaye hakuonekana kama mgombea mkuu Peter Kuwani inasemekana kajiapatia asilimia 2 ya kura hizo.
Mwaka uliopita, Malawi ilikuwa nchi ya pili barani Afrika kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais kutokana na kuibuka madai ya udanganyifu, baada ya Kenya 2017.
Mwandishi wa BBC katika eneo la kusini mwa Afrika, Andrew Harding anasema sio jambo la kawaida na kwa wengi linavutia
– Mahakama iliingilia kati na kubadilisha matokeo katika eneo ambalo wizi wa kura ni suala la nyeti.
Wafuasi wa Chakwera tayari wameanza kusherehekea kile wanachoamini ni ushindi wa kihistoria.
Katika kile kinachoaminika kuwa tukio la kwanza katika eneo la Sahara kwamba uchaguzi uliokumbwa na udanganyifu umebadilishwa na upinzani kuibuka na ushindi ukichukua madaraka kwa njia ya kidemokrasia.
Pongezi pia zimetolewa na viongozi wa upinzani katika mataifa ya Afrika ya Kusini.
“Maisha mapya kwa Malawi!,” alisema kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Nelson Chamisa.
“Mungu ameipatia Malawi Mcha Mungu”, aliongezea akitaja historia ya Chakwera kama kiongozi wa dini.
”Ndugu yangu, rafiki yangu na kiongozi ameshinda uchaguzi wa Malawi. Niliwasiliana naye kwa simu na kusherehekea ushindi wake”, alituma ujumbe wa twitter kiongozi wa zamani wa chama cha upinzani cha DA Mmusi Maimane.
Mwandishi wa BBC anasema taasisi za kidemokrasia nchini Malawi huenda zikakabiliwa na shinikizo kali katika saa chache na siku zijazo.
Taifa hilo lilikuwa limegawanyika kabla ya uchaguzi huo wa marudio huku kukiwa na maandamano makubwa ya kupinga serikali.
Kiongozi mkuu wa serikali amedaiwa kusema kwamba uchaguzi unaibiwa.
Watu walipiga kura siku ya Jumanne licha ya hofu ya corona
Akizungumza siku ya Jumanne baada ya kupiga kura kusini mwa Malawi, Mutharika alidai kumekuwa na ghasia katika maeneo ya upinzani.
”Inasikitisha, katibu wetu mkuu amepigwa . wale wanaosababisha ghasia hawana la kufanya ”, Reuters ilimnukuu Rais Mutharika akisema.
”Ni vipi sasa kwamba uchaguzi huu utakuwa wa haki na huru”?, alihoji.
Hatahaivyo ripoti hizo hazijathibitishwa.
Akipiga kura yake kiongozi wa upinzani Chakwera alisema kwamba ana imani na tume ya uchaguzi kufanya kile kilicho cha haki.
”Naamini kwamba hatua ya raia wa Malawi kutafuta haki inajibiwa hii leo. Na naamini haki yao itaheshimiwa”, aliongezea.
Yeyote yule atakayeibuka mshindi atalazimika kutibu mgawanyiko uliotokea pamoja na kukabiliana na masuala muhimu ya ufisadi, umasikini na ukosefu wa ajira.
Kura ya marudio ya uchaguzi wa Mei 2019 iliagizwa na mahakama ya kikatiba nchini Malawi mwezi Februari baada ya majaji kubaini udanganyifu mwingi.
Uchaguzi huo ulimfanya rais Mutharika kupata ushindi mwembamba wa kura 159,000 ambazo ni asilimia 38.6 ya kura zilizopigwa . Chakwera alikuwa wa pili akipata asilimia 35.4.
Chakwera na mgombea aliyekuwa katika nafasi ya tatu walihoji kwamba uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.
Malalamishi yao yalishirikisha madai kwamba nakala za kuhesabu kura hizo zilifutwa na kuongezewa idadi ya kura kwa kutumia wino wa kusahihisha makosa.
Hali ya sintofahamu kuhusu matokeo hayo ilizua miezi kadhaa ya wasiwasi na maandamano, yaliobadilika na kuwa ghasia kati ya wafuasi wa upinzani na maafisa wa polisi kote nchini.
Uamuzi wa mwezi februari wa kufuta matokeo hayo ya uchaguzi uliwafanya watu kusherehekea , lakini Mutharika alitaja uamuzi huo kama” mabadiliko ambayo yanaadhimisha mwanzo wa mwisho wa demokrasia nchini humo.
Mwezi uliopita, mwenyekiti wa zamani wa tume ya uchaguzi nchini Malawi, Jane Ansah alijiuzulu kufuatia miezi kadhaa ya shinikizo kutoka kwa waandamanaji ambao walimkosoa kwa jinsi alivyosimamia uchaguzi huo.
Kura mpya inajiri wakati ambapo kuna hofu kubwa kati ya serikali na mahakama za taifa hilo.