Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiongozi Burkina Faso azikwa baada ya miaka 36

Thomas Sankara.jpeg Kiongozi Burkina Faso azikwa baada ya miaka 36

Fri, 24 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabaki ya kiongozi wa zamani mwanamapinduzi wa Burkina Faso Thomas Sankara yalizikwa Alhamisi katika eneo alikouawa katika mapinduzi ya kijeshi zaidi ya miongo mitatu iliyopita.

Sankara alizikwa pamoja na wanamapambano wenzake 12 wa zamani katika eneo la Ukumbusho wa Thomas Sankara katika mji mkuu Ouagadougou.

Maafisa kadhaa wa serikali ya kijeshi wakiongozwa na Waziri Mkuu Apollinaire Kyelem walihudhuria sherehe hiyo ambayo ilisusiwa na familia ya Sankara.

Majeneza 13 yaliyokuwa na mabaki hayo yalipambwa kwa bendera ya taifa huku kila moja likiwa na picha ili viongozi watoe heshima zao kabla ya kuzikwa upya.

Viongozi wa kidini wa madhehebu tofauti walihimiza maridhiano ya watu wa Burkina Faso ili kufikia amani katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi inayokumbwa na ukosefu wa usalama.

Familia ya Sankara ilisema awali wasingehudhuria kwa sababu hawakuridhishwa na eneo hilo la maziko. Lakini serikali ilisema eneo hilo jipya la maziko limechaguliwa kwa kutegemea zaidi matakwa ya kijamii na kitamaduni, usalama na maslahi ya kitaifa. Thomas Sankara

Sankara, ambaye alichukua madaraka mwaka 1983, aliuawa Oktoba 15, 1987, wakati wa mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Blaise Compaore, mshirika wake wa zamani. Alikuwa na umri wa miaka 37 alipouawa.

Campaore naye aling'olewa madarakani mnamo 2014 katika mwamko wa wananchi baada ya miaka 27 madarakani.

Miili hiyo 13 ilitolewa kwenye makaburi nje kidogo ya mji mkuu kufuatia kuanguka utawala wa Compaore.

Uchunguzi wa mauaji ya Sankara ulipelekea kufunguliwa kesi ya watuhumiwa 14 waliotuhumiwa kupanga mauaji hayo na hatimaye walipatikana na hatia mnamo Aprili 2022 na kuhukumiwa vifungo vya miaka 3 hadi 35 jela. Aidha Compaore, ambaye anaishi uhamishoni Ivory Coast, alihukumiwa kifungo cha maisha bila kuwepo mahakamani.

Sankara, aliyepewa jina la utani la Che Guevara wa Afrika, alikuwa afisa wa kijeshi na mwanamapinduzi wa kisoshalisti. Anasalia kuwa mfano wa kuigwa na Waafrika wa mrengo wa kushoto kwa msimamo wake wa kupinga ubeberu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live