Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kinara wa maandamano apinga Rais kujiuzulu 

809e0b894fcc62ece017cfa4c82a895b Kinara wa maandamano apinga Rais kujiuzulu

Sat, 1 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KIONGOZI wa Waislamu anayeshawishi maandamano nchini Mali, Mahmoud Dicko amesema mgogoro nchini humo unaweza kumalizwa bila Rais Ibrahim Boubacar Keita kujiuzulu akionekana kutoa suluhisho lenye nafuu kuliko viongozi wengine wa upinzani.

Inasemekana waandamanaji 14 waliuawa katika maandamano yaliyoitikisa serikali ya nchi hiyo Juni mwaka huu na kuleta hofu kuwa mtikisiko huo utasababisha mapigano ya Waislamu wenye msimamo mkali huko Sahel, Afrika Magharibi.

Licha ya makubaliano yao na Keita kumaliza mzozo wao, bado viongozi wa eneo hilo na M5-RFP wanaosuka mpango wa maandamano hayo walimtaka Rais Keita kuondoka madarakani ingawa amegoma kukubaliana na matakwa yao.

Katika mahojiano na Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, Dicko mwenye ushawishi mkubwa nchini humo akiwa kinara wa maandamano hayo ingawa si mwanachama wa muungano huo, alionekana kuchukua hatua zilizoonekana kuwa na nafuu zaidi kwa Rais Keita ukilinganisha na Muungano wa M5-RFP.

“Nadhani tunaweza kutafuta suluhisho bila kwenda mbali kama kuondoka madarakani kwa Rais. Ukiachana na kujiuzulu kwake kuna mambo mengi yanayoweza kufanyika,” alisema.

Akijibu swali ikiwa ataridhia kubadilishwa Waziri Mkuu, Boubou Cisse ambaye amekuwa akilaumiwa anavyoshughulikia utatuzi wa maandamano hayo, Dicko alisema mabadiliko hayo hayawezi kutatua mgogoro lakini anaweza kuwa sehemu ya makubaliano kuelekea suluhu.

Hotuba za Dicko zinazoishutumu serikali ya Keita zimeshawishi waandamanaji na washirika kumuona mtu mwenye nguvu nyuma ya maandamano hayo huku washirika wa Keita wakiamini kuwa ni mtu muwazi ambaye anaweza kumaliza maandamano hayo.

Maelfu ya raia wa Mali wameandamana juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa wakiituhumu serikali kwa udhaifu na ufisadi. Mauaji ya waandamanaji yalichochea hasira dhidi ya Rais Keita.

Licha ya kuwa na mtazamo tofauti na viongozi wengine wa upinzani, Dicko aliendelea kusisitiza hakuna mpasuko upande wa upinzani.

Chanzo: habarileo.co.tz