Polisi nchini Malawi wamesema takriban watu 15 wamefariki na wengine 16 hawajulikani walipo kutokana na uharibifu uliosababishwa na dhoruba ya kitropiki Freddy.
Pamoja na kukatika kwa mawasiliano bado haijulikani ukubwa kamili wa uharibifu na idadi ya waliojeruhiwa.
Polisi wamesema watu wamekufa baada ya nyumba zao kuharibiwa na polisi katika Jiji la Blantyre wanahofia watu wamenasa chini ya vifusi.
Freddy ni mojawapo ya dhoruba kali zaidi kuwahi kurekodiwa katika ulimwengu wa kusini na imesababisha wiki za mvua zinazoendelea kunyesha nchini Msumbiji na Malawi.
Tathmini ya awali ya mashirika ya kibinadamu yanayofanya kazi nchini Msumbiji inasema kumekuwa na uharibifu mkubwa wa nyumba za watu na miundombinu katika zaidi ya nusu ya majimbo ya nchi hiyo.