Kwa mara ya pili ndani ya wiki kadhaa Kimbunga Freddy kimeendelea kusababisha maafa Nchini Msumbiji baada ya Mvua kubwa iliyoambatana na upepo kupelekea majimbo ya kati ya Zambezia, Manica na Sofala kuathirika zaidi.
Kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa Nchini humo (INAM), Kimbunga hicho Freddy kilipunguza mwendokasi wake kuelekea taifa hilo la kusini mwa Afrika na kilikuwa kilomita 60 (maili 40) kutoka pwani siku ya Jumamosi asubuhi.
Kimbunga hicho ambacho pia kiliikumba Msumbiji mnamo Februari 6 ni mojawapo ya dhoruba kali zaidi zilizorekodiwa katika ukanda wa Kusini.
Baada ya kudumu kwa takribani siku 34 mfululizo, mfumo wa hali ya hewa kutokana na Kimbunga hicho unatajwa kuvunja rekodi ya kimbunga cha kitropiki kilichodumu kwa muda mrefu zaidi.
Kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni, rekodi ya awali ilishikiliwa na kimbunga cha siku 31 mnamo 1994.
“Naona baadhi ya nyumba zimepasuliwa paa, madirisha yamevunjwa na mitaa imejaa maji. Inatisha sana,” alisema Massinge, Mfanyakazi katika shirika la ufadhili la mazingira.