Rais wa Malawi Lazarus Chakwera Jumatano alitangaza wiki mbili za maombolezo ya kitaifa kwa zaidi ya watu 200 waliofariki kutokana na Kimbunga Freddy, kilichoikumba nchi hiyo mapema wiki hii.
Hatimaye kimbunga hicho kilififia baada ya kusafiri kilomita 8,000 kuvuka bahari ya Hindi, na kubadilika mkondo wake na kupiga Afrika kwa mara ya pili na kuweka rekodi isiyo rasmi ya dhoruba ndefu zaidi ya kitropiki duniani.
“Kutokana na idadi kubwa ya vifo vilivyosababishwa na maafa haya, nimeagiza kuwa sisi wote kama kama taifa, tutenge siku 14 za maombolezo na bendera zote zitapepea nusu mlingoti kwa siku saba za mwanzo,” rais huyo wa Malawi, alisema katika hotuba ya taifa kwa njia ya televisheni.
Kimbunga Freddy kiliacha athari za vifo na uharibifu. Nchini Malawi kimbunga hicho kimeua takriban watu 225, na kujeruhi mamia ya watu na wengine 41 hawajulikani walipo kulingana na takwimu rasmi. Wakati mafuriko na maporomoko ya udongo yakizisomba na kuzizika nyumba zao.
Siku ya Jumatano, juhudi za uokoaji zilikuwa bado zikiendelea huku matumaini ya kuwapata manusura yakipungua.
Chakwera alisema mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri umeidhinisha kutolewa kwa kwacha bilioni 1.6 sawa na dola milioni 1.5 kusaidia maelfu ya raia walioathiriwa na dhoruba.
Rais alisema Malawi ni moja ya nchi maskini sana duniani, inaomba misaada ya ziada kutoka jumuiya ya kimataifa.
"Naomba misaada zaidi kutoka kwa washirika wa kimataifa na wafadhili kwa ajili ya kukabiliana na uharibifu uliosababishwa na kimbunga cha kitropiki cha Freddy," rais Chakwera alisema alipohudhuria mazishi ya baadhi ya waathirika katika mji wa kusini wa Blantyre.