Kikosi cha Radiamali ya Haraka cha Sudan (RSF) kimewaachia huru watu 100 waliokuwa wamekamatwa mateka na jeshi la nchi hiyo. RSF kimesema kuwa kimewaachia huru watu hao kwa mnasaba wa Sikukuu ya Idul Adh'ha.
Kikosi cha RSF kimetangaza kuwa uongozi wao umeamua kuwaachia huru mateka 100 wa jeshi la Sudan. Mamlaka husika ya Sudan ilitangaza jana kuwa itaendelea kutekeleza amri ya kutotoka nje ambayo ilitangazwa kuanzia juzi Jumatatu.
Katika upande mwingine, Muhammad Hamdan Dagalo kamanda wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF) juzi usiku alitangaza kuwa watatekeleza usitishaji vita wa upande mmoja kwa siku mbili kwa mnasaba wa Sikukuu ya Idul Adh'ha. Aliongeza kusema kuwa, sikukuu hii Itakuwa fursa ya kuvumiliana kufikia maridhiano baina ya wananchi wa Sudan.
Kikosi cha RSF pia kimetangaza kuakhirisha mazungumzo ya Jeddah kati yake na jeshi la Sudan hadi baada ya Sikuu ya Idul- Adh'ha.
Sudan ilikumbwa na mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na askari wa kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF) wanaoongozwa na Kamanda Muhammad Hamdan Dagalo kuanzia Aprili mwaka huu. Mapigano hayo yamekuwa yakijiri katika mji mkuu Khartoum na katika miji mingine ya kaskazini na magharibi mwa nchi.
Mapatano ya kusimamisha mapigano yametangazwa kwa mara kadhaa huko Sudan hadi sasa hata hivyo pande zinazopigana zimekuwa zikikiuka mapatano hayo mara kwa mara.