Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikosi cha EAC chaanza kuondoa wanajeshi wake DRC

Vikosi UN Na Drc.jpeg Kikosi cha EAC chaanza kuondoa wanajeshi wake DRC

Mon, 4 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) kimeanza kuwaondoa askari wake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Msemaji wa kikosi hicho amesema kundi la kwanza la wanajeshi 100 kutoka Kenya, Uganda, Burundi na Sudan Kusini mapema leo limeabiri ndege katika Uwanja wa Ndege wa Goma, mashariki mwa DRC na kuelekea Nairobi, mji mkuu wa Kenya. Hata hivyo afisa huyo wa EACRF hajatoa maelezo zaidi kuhusu shughuli hiyo.

Mwezi Oktoba mwaka huu, msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya aliziambia duru za habari kwamba, serikali ya nchi hiyo haitawapatia kandarasi mpya wanajeshi hao wa kieneo wa EACRF.

DRC ilitangaza msimamo huo baada ya muungano wa vyama vya kiraia nchini Kongo DR kufanya maandamano mjini Goma ukitaka kikosi hicho cha pamoja cha Afrika Mashariki kuondoka mashariki mwa nchi hiyo, kutokana na kushindwa kukabiliana na waasi wa M23.

Mwezi Novemba mwaka jana, Kenya, Burundi, Uganda na Sudan Kusini zilituma wanajeshi wao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, chini ya bendera ya Jeshi la Kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF), kujaribu kulipokonya silaha kundi hilo la waasi na kuleta amani.

Wanajeshi wa EAC walipowasili mashariki mwa DRC mwaka mmoja uliopita Waasi wa M23 wanaoongozwa na Watutsi walifanya mashambulizi mwishoni mwa 2021 na kuteka maeneo ya Kivu Kaskazini, mbali na kusababisha zaidi ya watu milioni moja kukimbia makazi yao. Kundi hilo limeendelea kushikilia baadhi ya miji na vijiji katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Eneo la mashariki mwa DRC limekumbwa na mizozo na mapigano kwa takriban miaka 30 sasa, kutokana na harakati za makundi ya waasi wenye kubeba silaha, ya ndani na nje ya nchi hiyo.

Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kusaini makubaliano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhusu kuondoka kwa ujumbe wa umoja huo wa kulinda amani nchini humo (MONUSCO). Hayo yalisemwa karibuni na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo DR, Christophe Lutundula ambaye alieleza kuwa, makubaliano yaliyosainiwa baina yake na Mkuu wa MONUSCO yanaashiria mwisho wa ushirikiano wa pande mbili ambao umeshindwa kuzaa matunda mashariki mwa DRC kwa zaidi ya miongo miwili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live