Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikao cha marais EAC sasa chanukia

01b675de862c16c153ae72620baf7cb5.png Kikao cha marais EAC sasa chanukia

Tue, 16 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUTANO unaosubiriwa kwa hamu wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umependekezwa kufanyika Februari 27, mwaka huu.

Katibu Mkuu wa EAC, Liberat Mfumukeko amependekeza kikao hicho cha Baraza la Mawaziri, kifanyike Februari 25, mwaka huu.

Alisema hayo katika barua yake kwa makatibu wakuu na mawaziri wanaoshugulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

"Kufuatia mashauriano na Mwenyekiti wa Baraza, napenda kuitisha mkutano wa 40 wa kawaida wa Baraza la Mawaziri kuanzia Februari 22-25, 2021 Arusha, Tanzania."

"Pia tunapendekeza mkutano wa kawaida wa 21 wa wakuu wa nchi wa EAC ufanyike Jumamosi Februari 27, mwaka huu," alisema Mfumukeko.

Mkutano huo utakuwa na vikao kadhaa ambavyo vitajumuisha maofisa wakuu wa serikali na makatibu wakuu kuanzia Februari 22 na kuishia kwa mkutano wa Baraza la Mawaziri Februari 25.

Uteuzi wa Katibu Mkuu ajaye wa EAC, unatarajiwa kuwa ajenda kuu ya mkutano huo.

Masuala mengine yatakayojadiliwa ni uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na mipango ya miundombinu kwa kipindi cha 2021-24.

EAC pia imeweka kipaumbele katika mipango ya kufufua uchumi, ambao umeathiriwa na hatua na kanuni za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

"Nchi washirika wa EAC zinaangalia jinsi ya kukabiliana na athari za virusi vya corona kwenye uchumi wa ukanda mzima,"alisema Waziri wa Nchi wa Rwanda anayesimamia EAC, Nshuti Manase ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kuna mambo tunayohitaji kufanyia kazi pamoja hususan uhuru katika muingiliano wa bidhaa na watu. Tunahitaji kuona kuwa usafirishaji wa bidhaa unaendelea bila vikwazo na Umoja wa Forodha unafanya kazi,” alisema.

Mratibu wa Habari katika Sekretariati ya EAC, Florian Mutabazi alisema kwa sasa wanaandaa mkutao wa Baraza la Mawaziri na baada ya marais wa nchi, kuthibitisha ndiyo kitaandaliwa kikao cha viongozi wakuu wa nchi.

Chanzo: habarileo.co.tz