RAIS Salva Kiir ameunda kamati maalumu ya kukabiliana na mdororo wa kiuchumi uliopo kwa sasa itakayoongozwa na Makamu wake wa Rais anayeshughulikia uchumi, James Wani Igga.
Moja ya majukumu ya kamati hiyo ni kuweka mikakati itakayowezesha kuimarika kwa mapato yasiyotokana na mafuta ili kuongeza mapato ya nchi hiyo yaliyoathiriwa na vita, maambukizi ya virusi vya covid-19 na kushuka kwa bei ya mafuta ulimwenguni.
Wajumbe wa kamati hiyo ni mawaziri wa fedha, biashara na viwanda, mafuta na madini. Wengine ni Gavana wa Benki Kuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato ya Taifa, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Juba na Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Kuundwa kwa kamati hiyo kumekuja siku chache baada ya Benki Kuu ya nchi hiyo kutangaza imeishiwa fedha za kigeni na kuongezeka kwa vitendo vya rushwa katika taasisi za fedha.