Alifahamika kama ‘mpishi wa Putin’ na bilionea, kiongozi na muasisi wa kundi la askari wa kukodiwa la Wagner, linaloendesha mapigano na ushawishi wa Russia katika nchi za Afrika.
Yevgeny Prigozhin (62), amefariki dunia siku tatu zikizopita akiwa kwenye ndege iliyotunguliwa. Utajiri wake ni wa Dola 1 bilioni za Marekani (Sh2.5 trilioni).
Je, kifo cha Prigozhin ndiyo salama ya nchi za Afrika? Ndiyo itakuwa mwisho wa matumizi ya wanajeshi wa kundi la Wagner wanaoshutumiwa kwa uhalifu wa kivita, kama vile wizi, ubakaji na mateso?
Prigozhin na Wagner
Mfanyabishara Prigozhin, ndiye mwanzilishi wa kundi la Wagner likiwa kampuni binafsi ya kijeshi inayohusishwa na Serikali ya Russia.
Inakadiriwa kuna wanajeshi takriban 5,000 wa kundi la Wagner walioko kote barani Afrika, mchanganyiko wa wanajeshi wa zamani wa Russia, wafungwa na raia wa kigeni.
Tangu mwaka 2014, Prigozhin amekuwa kiongozi wa kundi la Wagner ambalo limekuwa likiingilia kati masuala ya nchi kadhaa za Afrika, likitoa msaada wa kijeshi na usalama; huku likipanua ushawishi wa Russia katika Bara la Afrika.
Wagner chini ya Prigozhin limefanya kazi katika nchi kadhaa za Afrika tangu mwaka 2017, mara nyingi huwapa wateja wake msaada wa moja kwa moja wa kijeshi, huduma zinazohusiana na usalama; pamoja na kueneza propaganda za Russia. Prigozhin siku chache kabla ya kifo chake imeelezwa alikuwa nchini Mali ambako kundi hilo linatoa huduma ya ulinzi na usalama na hulipwa kwa mwaka Euro 103 milioni, sawa na Sh278.5 bilioni. Vita katika nchi za Mali na Afrika ya Kati zinaelezwa kuchangiwa na kundi la Wagner chini ya Prigozhin.
Ingawa askari wa kukodiwa ni kinyume cha sheria nchini Russia, Serikali imekuwa ikilitumia kundi la Wagner kusambaza ushawishi wenye masilahi yake ya sera za kigeni barani Afrika.
Pia, kundi la Wagner lilijihusisha barani Afrika kwa sababu zake, kama vile kutengeneza fedha. Mwaka huu Marekani imelitaja kundi hilo kama shirika kubwa la uhalifu la kimataifa.
Kundi la Wagner limeshiriki mapigano katika nchi kadhaa za Afrika, zikiwamo Jamhuri ya Afrika ya Kati, Libya, Mali na Sudan, ambazo zote zina uhusiano mbaya na nchi za Magharibi.
Wanafanya nini Afrika
Huduma za Wagner hutofautiana kulingana na mahitaji ya wateja wake, ambayo ni pamoja na vikundi vya waasi na Serikali, pia ufadhili wake ni kati ya malipo ya moja kwa moja au makubaliano ya rasilimali. Mfano, operesheni za wanajeshi wa Wagner zimeunga mkono Serikali za Afrika katika kupambana na makundi ya waasi na yale ya kigaidi.
Takriban wanajeshi 1,000 wa Wagner waliingia Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2018 kutetea Serikali ya Rais Faustin-Archange Touadera dhidi ya mashambulizi ya waasi kwenye mji mkuu, Bangui. Pia, nchini humo kampuni za Wagner zilipokea haki za ukataji miti bila vikwazo na udhibiti wa mgodi wa dhahabu wa Ndassima.
Wagner Msumbiji
Vikosi vya Wagner vilitumwa Msumbiji mwaka 2019 kusaidia kupambana na wapiganaji wanaojiita Islamic State katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado. Hata hivyo, kundi hilo lilishindwa kuzuia uasi na kujiondoa katika eneo hilo baada ya miezi michache.
Kundi la Wagner pia hutoa huduma ya usalama kwa Serikali zilizo hatarini kuanguka. Mfano, kikundi hiki kilitumika kama sehemu ya ulinzi binafsi kwa Rais Touadera na kusaidia kutoa mafunzo kwa Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati kujiandaa kwa majaribio ya mapinduzi yanayoweza kutokea.
Pia, Wagner wamekuwa wakifanya kazi nchini Sudan tangu 2017, wakitoa mafunzo kwa wanajeshi kulinda rasilimali za madini na kukandamiza upinzani dhidi ya Serikali ya Rais Omar al-Bashir (kwa sasa ameondolewa madarakani). Yote hayo ikiwa ni kubadilishana na mauzo ya dhahabu kwenda Russia.
Msaada wa Wagner huongezewa na usaidizi rasmi wa kijeshi wa Russia, kama vile nchini Mali, ambako vikosi vya jeshi vilipokea ndege za kivita na uchunguzi kutoka Moscow.
Askari ‘kivuli wa Putin’
Kundi la Wagner kwa namna linavyoenea barani Afrika, linafahamika kama mamluki wa Russia. Pia huchimba almasi, hueneza propaganda na kuwaunga mkono watawala. Kulingana na ripoti ya taasisi ya Acled, Zimbabwe iliorodheshwa namba tano, wakati shughuli za Wagner zimeripotiwa duniani kote.
Shughuli za kundi hilo barani Afrika zimeripotiwa katika maeneo ya nchi za Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati, DRC, Angola, Zimbabwe, Madagascar, Msumbiji, Sudan na Libya.
Watafiti, Kituo cha Afrika cha Mafunzo ya Kimkakati katika ripoti iliyopewa jina la ‘kufuatilia uingiliaji wa Russia katika kuondoa demokrasia barani Afrika’ inaeleza namna Taifa hilo lilivyokuwa likiisaidia Zanu PF kushikilia madaraka.
Juni 27, mwaka huu, ripoti ya Idara ya Hazina ya Marekani imeibua wasiwasi kuhusu shughuli za kundi la Wagner nchini Zimbabwe na nyingine za Afrika.
Taarifa hiyo inasema Marekani ilikuwa ikitoa ushauri kwa kuzingatia ongezeko la ripoti kuhusu jukumu la watendaji haramu katika biashara ya dhahabu, ikiwa ni pamoja na kundi la Wagner na kuangalia fursa na hatari zilizoletwa na biashara ya dhahabu katika nchi za kusini mwa Afrika.
Wanashirikiana na viongozi wenye migogoro na makamanda wa wanamgambo wanaoweza kulipia huduma zao kwa fedha taslimu au kwa makubaliano ya faida ya uchimbaji madini ya thamani kama dhahabu, almasi na urani.
Kundi la Wagner linajihusisha na siasa, linaunga mkono watawala wa Serikali na kuandaa kampeni za propaganda za kidijitali. Linatoa chakula kwa masikini na linazalisha sinema za maigizo zilizowekwa barani Afrika.
Lilikotoka jina Wagner
Wagner iliibuka wakati wa shambulio la kwanza la Russia dhidi ya Ukraine mwaka 2014, wakati mamluki hao walipopigana pamoja na watu wanaounga mkono Taifa hilo kujitenga katika eneo la Donbas.
Kiongozi wake alikuwa Dmitry Utkin, kamanda mstaafu wa kikosi maalumu cha Russia anayesemekana kuvutiwa na historia na utamaduni wa Wanazi.
Jina la kikundi, na ishara ya wito wa kijeshi wa Utkin, limechukuliwa kwa mtunzi Richard Wagner, kipenzi cha Hitler. Baadhi ya wapiganaji wa kundi hilo wana itikadi hiyo: Alama za kale za Norse zinazopendelewa na watu weupe wenye msimamo mkali zimepigwa picha kwenye vifaa vya Wagner barani Afrika na Mashariki ya Kati.
Mpishi wa Putin
Prigozhin alifahamika kama mpishi wa Putin (Vladimir Putin), kwa kuwa katika miaka ya 1990 alikuwa na mgahawa ambao Putin alipenda kwenda kupata chakula.
Putin alipokuwa Rais wa Russia, kampuni ya Prigozhin ya Concord Catering, ikapewa zabuni ya kutoa huduma ya chakula cha mchana kwenye shule, jeshi na magereza, hali iliyomfanya awe bilionea.
Prigozhin aliendesha mtandao wa kampuni kadhaa, zikiwamo zinazotuhumiwa kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka wa 2016 na 2018.