Kesi ya mshukiwa wa ufadhili wa mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994 imesitishwa huko The Hague.
FĂ©licien Kabuga, ambaye ana umri wa miaka 90, alikuwa akikabiliwa na kesi baada ya kukwepa kukamatwa kwa miaka 26, lakini mawakili wake wanasema ana shida ya akili na hastahili kushtakiwa.
Kesi hiyo imesitishwa kupisha afya yake iweze kutathiminiwa.
Anadaiwa kuwafadhili wanamgambo wa kabila la Hutu ambao waliwachinja Watutsi wapatao 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Mauaji hayo yalifanyika kwa muda wa siku 100 pekee. Inadaiwa kuwa alitumia utajiri wake mkubwa alioupata katika biashara ya chai miaka ya 1970 kununua mapanga yaliyotumika kuwapa silaha wauaji wa Wahutu.
Mfanyabiashara huyo tajiri pia anatuhumiwa kutumia kituo chake cha redio kuwahimiza Wahutu kuwaua Watutsi hasimu, na hivyo kuchochea mauaji ya halaiki kwa kutangaza matamshi ya uchochezi ya chuki.
Amekana mashtaka yote. Bw Kabuga alikamatwa mwaka wa 2020 baada ya kushindwa kukamatwa kwa miongo kadhaa.
Wachunguzi wa Ufaransa walimtafuta hadi kwenye ghorofa moja huko Paris ambako alikuwa akiishi akiwa na utambulisho wa uongo.
Manusura wa mauaji ya halaiki hapo awali wameelezea wasiwasi wao kwamba haki huenda isitendeke ikiwa Bw Kabuga atafariki bila kukabiliwa na kesi katika mahakama ya ICC, ambayo tayari ilitarajiwa kuchukua miaka kadhaa.