Kesi ya muda mrefu ya rushwa inayomkabili Rais wa zamani wa Afrika Kusini aliyeko jela Jacob Zuma itaendelea leo kwa njia ya video licha ya Vurugu kali ambazo zimelikumba taifa hilo.
Zuma anakabiliwa na mashitaka 16 ya ulaghai na rushwa kuhusiana na ununuzi wa ndege za kivita mwaka 1999, boti za kushika doria na vifaa vya Jeshi kutoka kwa kampuni tano za kijeshi Ulaya wakati akiwa Naibu wa Rais.
Anatuhumiwa kupokea hongo kutoka kwa moja ya kampuni hizo, Thales ya Ufaransa ambayo ilishitakiwa kwa rushwa na utakatishaji pesa.
Kesi hiyo ilianza May 2021 baada ya kuahirishwa na kucheleweshwa mara nyingi, wakati timu ya utetezi ya Zuma ikipambana kutaka mashitaka hayo yafutwe ambapo Zuma mwenye umri wa miaka 79 anasisitiza hana hatia huku Kampuni ya Thales pia ikikana tuhuma hizo.