Kazi imeanza, ndivyo unavyoweza kusema juu ya uamuzi wa Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyata kuamua kuendelea kuwa kiongozi wa chama cha Jubilee huku akiweka wazi asiyekubaliana na uamuzi wake ruksa kuondoka.
Uamuzi huo unamfanya aendelee kuwa kwenye siasa za kila siku akipambana na Rais William Ruto aliyeshinda katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 29, 2022 dhidi ya Raila Odinga (Azimio la Umoja)aliyeungwa mkono na Kenyatta
Hatua hiyo pia inazima jaribio la kumuondoa ndani ya chama hicho lililofanywa wiki tatu zilizopita na baadhi ya wanachama wa Jubilee waliopachikwa jina la ‘wasaliti.’
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Jubilee, uliofanyika jana Kenyatta alisema uamuzi wa kuiacha nafasi hiyo ndani ya chama hicho utatokana na matakwa ya waliomchagua.
Alisema waliompa uongozi walimpa na miongozo ya utendaji na alifanya kadri ya uwezo wake kuitekeleza, hivyo watakapomtaka ampishe mwingine atafanya hivyo.
Harakati za kumuondoa kiongozi huo ndani ya Jubilee, ziliongozwa na Kaimu Katibu Mkuu, Kanini Kega ambaye Mei 3, 2023 aliongoza kikao kilichoamua kumuondoa Kenyatta kwa kile kilichoelezwa kuwa tamati ya uongozi wake imefika kwa mujibu wa Katiba.
Alidai Ibara ya 6 (1) ya Katiba ya Kenya inamtaka Rais anayestaafu kutoshika nafasi yoyote ya uongozi wa chama cha siasa kwa zaidi ya miezi sita baada ya kustaafu.
Sabina Chege alichaguliwa kurithi nafasi hiyo ambayo hata hivyo amedumu nayo kwa wiki tatu hadi jana alipokosa baraka za wajumbe wa mkutano wa Jubilee.
Msimamo wa Kenyatta, uliambatana na uamuzi wa hatima ya uongozi wa Kega katika chama cha Jubilee kwa nafasi ya Kaimu Katibu Mkuu, baada ya mkutano mkuu wa chama hicho kuazimia kumvua wadhifa huo.
Pamoja naye, wengine waliopoteza uongozi ni Jimi Angwenyi, Naomi Shabban, Joshua Kutuny, Mutava Musyimi na Rachel Nyamai.
Uamuzi wa kuondolewa kwao, umetokana na kile kilichofafanuliwa na Kenyatta kuwa ni sehemu ya mikakati ya kukinyoosha na kukifufua chama hicho.
Kuvuliwa kwao kunatokana na kile kilichoelezwa ni kushirikiana na upande wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais Ruto.
Akihutubia Mkutano wa wanachama wa Jubilee nchini Kenya jana, Kenyatta alitupa kijembe kuwa uongozi wake hautakoma hadi watakapoamua waliomchagua.
Mwanasiasa huyo alichaguliwa tena na Baraza Kuu la Jubilee kukiongoza chama hicho, Februari 26, mwaka jana, siku hiyo hiyo lilitangaza kusitisha uhusiano na chama cha UDA cha Ruto.
Katika hotuba yake mbele ya wana Jubilee, Kenyatta alisema ingawa alikuwa na fikra za kuachana na shughuli za kisiasa, wengine walimtaka kufanya hivyo kwa vitisho.
“Wengine wameamua kazi itakuwa ya vitisho na kulazimisha, siku ya leo (jana) nimewaambia tafuteni mwingine sio Uhuru wa Kenyatta,” alisema na kuibua shangwe kutoka kwa wanachama hao.
“Tukamaliza kwa amani na tukapatiana uongozi kwa amani wajameni, hadharani mchana, hata wakati wananitukana nilikaa kimya nikasema acha watende yale wanaona haki yao kuyafanya.
“Nikakaa kimya na yale yametokeza tu matusi, kuiba mbuzi, kuchoma mashamba, yote wakifikiria wanatisha, haya nawaambia waendelee lakini chama sio cha Uhuru kina wenyewe na wenyewe walinipatia niichunge.
“Na mpaka wataniambia wapo tayari wamechagua mwingine, nitashikiria mpaka wataniambia sasa muachie mwingine,” alisema.
Alisema haitokani na hasira wala chuki bali ni heshima kubwa akidokeza; “Inasemekana ukitaka kuheshimiwa lazima uheshimu wenzako.”
Kinachomshangaza ni kile alichokieleza kuwa, baadhi ya wanasiasa waliopata dhamana za uongozi ndani ya Jubilee wanataka kukifanya chama hicho kama wanavyotaka.
“Jukumu lao lilikuwa ni kutetea sera, ilani za wana Jubilee na kama hawawezi wakae kando tutaweka wengine. Sisi ni watu tunaopenda amani, lakini kupenda amani sio kusema wewe ni muoga, tukitaka kuongea tuongee kwa heshima,” alisema.
Alitaka kila mwanachama kuhakikisha anakijenga chama hicho kuanzia ngazi ya shina, huku akionya matusi isiwe lugha itakayotumiwa nao.
“Kuona wengine wamenyamaza sio eti wameogopa, mjiheshimu kama viongozi, mtaheshimika. Wengi wetu tunaamini mwishowe haki lazima itatendeka kwa sababu Mungu bado yupo na halali, wale wakifikiria kwamba Mungu analala, Mungu halali,” alisema.
Kwa mujibu wa Kenyatta, wanasiasa wasiofurahishwa na msimamo wa Jubilee, wanapaswa kutafuta namna ya kuondoka kwenye chama hicho.
“Mnasema chama chetu kimekufa, nani ana haja na maiti kama kimekufa kwa nini mnang’ang’ania si ni maiti jamani, ukiona wanakitafuta ni kwa sababu tupo hai,” alisema.