Rais mteule wa Kenya William Ruto anasema Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta hajaona inafaa kumpongeza kwa ushindi wake katika uchaguzi huo.
"Nimeshinda uchaguzi, hilo ndilo la muhimu...Bahati mbaya Rais Kenyatta hajaona inafaa kunipongeza lakini nadhani ni sawa, labda amekatishwa tamaa, au hafurahii kwamba nilimshinda mgombea wake. Lakini hivyo ndivyo siasa ilivyo,” aliiambia CNN.
Mahojiano hayo yalipeperushwa saa chache baada ya Bw Ruto kuweka mtandaoni kuhusu mazungumzo yake ya simu na Rais Kenyatta, ambapo walijadili kuhusu uchaguzi mkuu na shughuli ya mpito kwa utawala mpya.
Bw Ruto, ambaye ni Mkristo muinjilisti, pia aliambia CNN kwamba haki za wapenzi wa jinsia moja "si suala kubwa" nchini kwa sasa, na ataangazia masuala muhimu zaidi ya ukosefu wa ajira na njaa.
‘’Hatutaki kukuza kitu kisicho na umuhimu kukifanya kionekane kuwa na umuhimu mkubwa. Hili si suala muhimu kwa watu wa Kenya.’’
Aliongeza: "Suala la mapenzi ya jinsia moja na haki zao litakapokuja, watu wa Kenya watafanya uchaguzi na tutaheshimu chaguo zao. Kwa sasa tuangazie masuala yanayoathiri watu wetu."
Sheria ya enzi za ukoloni inaharamisha mapenzi ya jinsia moja nchini Kenya - ambayo ni adhabu ya kifungo cha hadi miaka 14 jela.
Haijabainika iwapo kumewahi kuwa na hatia ya kufanya mapenzi ya jinsia moja nchini Kenya.