Nachelea kusema huenda sasa ni wakati mgumu Zaidi kwenye maisha ya kisiasa ya Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Ni wakati ambao kila mtu aliyekuwa anamuamini ndani na nje ya chama chake cha Jubilee anamtilia shaka na kuhisi labda hafai tena kuongoza chama hicho.
Jumapili nilimsikiliza mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya chama cha jubilee, Sabina Chege ambaye pia alikuwa karibu na Uhuru Kenyatta akimrushia maneno kiongozi wake huyo wa chama na kumtaka atoe msimamo juu ya yanayoendelea kwenye muungano wa Azimio la Umoja ambao unafanya maandamano kadhaa. Also Read
Nida yatakiwa kuharakisha utoaji vitambulisho Kitaifa 1 hour ago Nida yatoa ruksa kubadilisha kitambulisho kwa kulipia Kitaifa 1 hour ago
Kwa upande mwingine maandamano hayo yanayoongozwa na Raila Odinga ambaye ni kiongozi wa muungano huo yanaonekana kutoungwa mkono na wafuasi wengi wa Jubilee.
“Tukiwa msibani kwa George Magoha (aliyekuwa waziri wa elimu wa Kenya) tulishangaa kuona Kenyatta akipanda kwenye gari lake huku akisema kiongozi wake ni Raila Odinga. Tunamtaka atoke hadharani aseme msimamo wa chama chetu kwa sasa,”alisema.
Wakati vuguvugu na sintofahamu ikiendelea ndani ya chama cha Jubilee, pia wale wabunge 30 wa Azimio la Umoja (wakitokea Jubilee) waliokutana na Rais William Ruto, wametangaza mpango wao wa kujitoa kwenye umoja wa Azimio la Umoja unaoongozwa na Raila Odinga.
Katika duru za siasa, bila kigugumizi unaweza kusema kiongozi wa umoja wa Kenya Kwanza na Rais wa tano wa nchi hiyo, William Ruto anahusika katika vuguvugu hizo ndani ya chama cha Jubilee kwasababu sasa hivi anaendelea kuitafuta nguvu ya kisiasa kwa kuwa na wabunge wengi wanaomuunga mkono.
Turudi kwenye hoja yetu, je, Ruto ni Rais wa kwanza wa Kenya kufanya hivi? La hasha kitu kama hiki pia kilifanyika na Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliuleta karibu upinzani ulioongozwa na Raila Odinga na kuungana nao na hata akakosa wabunge walio kinyume nae kimtazamo.
Hii ilimsaidia kupata ushirikiano mkubwa kwenye kupitisha masuala yake bungeni kwasababu alipata ‘sapoti’ ya upinzani na kitendo hichi, William Ruto ambaye wakati wa kampeni za kugombea urais alilizungumzia sana jambo hili kuwa liliua upinzani wa Kenya.
“Katika utawala wangu, nitaruhusu upinzani uwepo na sitafanya maridhiano ili usaidie kuikosoa Serikali,”alisema Ruto mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Kwahiyo, hali inayomkuta Kenyatta kwasasa ni kama ‘upanga aliutumia kuua wakati wa utawala wake umemrudia na unamuua yeye mwenyewe’ maana aliungana na upinzani na alifanikiwa kuufunga mdomo.
Na sasa yeye amekuwa mpinzani na wabunge wake 30 wanaelekea kuunga mkono juhudi na sasa wanashawishi wanachama wengine wa chama cha Jubilee wajitoe kwenye umoja huo.
Geofrey Mlwilo, Mchambuzi wa siasa za Kenya anasema ni wakati ambao Kenyatta anapaswa kukaa chini na wanachama wake wa Jubilee na kuona hitaji lao kubwa kwa sasa lipo wapi.
“Katika hali ambayo chama cha Jubilee inakipitia kwa sasa ni vyema wakutane na waone kwa sasa wanataka nini? Je, kuendelea kuwepo kwenye muungano wa Azimio la Umoja au kusimama wenyewe,”anasema.
Mlwilo aliongeza kuwa kwa uzoefu wa Kenyatta kwenye siasa za nchi hiyo ni rahisi kwake kutatua mgogoro huo endapo ataangalia chanzo cha mgogoro huo na hitaji sahihi la Jubilee wakati huu lipo wapi.
Josiah Mutabhuzi, mtaalamu wa Sayansi ya Siasa anasema mvutano anaokutana nao Kenyatta kwasasa unatokana na aina ya maisha ambayo amechagua kuyaishi baada ya kutoka madarakani.
“Unajua ukifuatilia marais wengi wa Kenya wakimaliza muda wao wa uongozi wanakaa pembeni na masuala ya siasa, sasa kwa upande wa Kenyatta ni tofauti naona bado anaendelea na propaganda na mikutano ya hadhara ya kisiasa hili lazima lilete joto flani,”alisema.
Mutabhuzi aliongeza kuwa katika siasa kuna muda unapoteza nguvu ya siasa na kuaminika na unachotakiwa kufanya ni kukaa kimya kwa muda au kufanya mambo ambayo wafuasi wako wanayaamini kuwa yapo sahihi.
Kwa yanayoendelea Kenya baina ya Kenyatta na wafuasi wake lakini pia Ruto na Kenyatta moja kwa moja yanashabihiana na maneno ya mwanafalsafa maarufu wa Ujerumani, Imanuel Kant aliyesema ‘mfanyie mwenzako unayopenda kufanyiwa’.
Kenyatta akiwa madarakani aliyafanya ambayo yeye hapendwi kufanyiwa, Kamba aliyotumia kuwanyonga wenzake nay eye inamnyonga kwasasa.
Kenyatta aliingia rasmi kwenye siasa za Kenya mwaka 1997 baada ya kugombea ubunge kwenye jimbo la Gatundu Kusini na kushindwa.
Kenya wana Bunge la Seneti na Bunge la Kitaifa ambapo katika uchaguzi wa Agosti 2022, muungano wa Azimio la Umoja unaoongozwa na Raila Odinga akiungwa mkono na Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta ulikuwa na wabunge wengi Zaidi na wale wa Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto.
Azimio la Umoja ulikuwa na wabunge 162 huku Kenya Kwanza kikiambulia wabunge 152 tu huku wengine 10 wakiwa hawana chama, pasi na shaka suala hili lilikuwa zuri kwa upande wa Odinga na Kenyatta lakini pia lilikuwa chungu kwa upande wa Ruto, kwasababu ingemkwamishia kupitisha mambo yake mengi.
Mpaka sasa hali ni shwari kwa Odinga na Kenyatta Ruto baada ya wabunge 10 wasio na chama kumuunga mkono Ruto na kuhamia muungano wa Kenya Kwanza, wabunge 30 wa Azimio la Umoja pia kuonyesha kumuunga mkono hivyo kwa hesabu za haraka mpaka sasa katika Bunge la Kitaifa ana wabunge 192 wanaomuunga mkono huku Kenya kwanza ikisalia na wabunge 132 tu.