Rais Mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta, amesema kwamba maafisa wa polisi waliofika nyumbani kwa mwanae Jomo siku ya Ijumaa usiku walikuwa na lengo la kupandikiza silaha haramu pamoja na madawa ya kulevya.
Kufuatia sakata la familia hiyo kutakiwa kurudisha silaha 28 inazozimiliki kwa mamlaka husika, Kenyatta amesema watoto wake wawili wa kiume ndiyo wanaomiliki silaha sita ambazo zimesajiliwa kwa mujibu wa sheria
"Suala hili la silaha lina propaganda nyingi ili kugeuza mawazo kutokana na kile ambacho kimekuwa kikitokea, ninaamini walitaka kupandikiza dawa za kulevya na bunduki kwenye nyumba ya mwanangu," amesema Kenyatta
Aidha Kenyatta ameongeza kwamba mpaka sasa hakuna mwanaye aliyepokea agizo la kusalimisha silaha zake kama ambavyo inaripotiwa kwenye vyombo vya habari.