RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameahidi kuhakikisha umoja na mafanikio zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakati anachukua uenyekiti wa jumuiya hiyo.
Amesema atafanya juhudi kubwa kutimiza matakwa ya pamoja, yaliyofufua jumuiya hiyo miaka 20 iliyopita.
Rais Kenyatta amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano wa kawaida wa 21 wa wakuu wa nchi za jumuiya hiyo, uliofanyika Jumamosi iliyopita kwa njia ya mtandao kutokana na janga la corona.
Amekuwa Mwenyekiti wa EAC baada aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame kumaliza muda wake.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Rais Kenyatta alitoa heshima kubwa kwa marais wa zamani, Daniel arap Moi (Kenya) na Benjamin Mkapa (Tanzania) na Rais wa sasa wa Uganda, Yoweri Museveni kwa hatua walizochukua katika kuanzisha upya EAC miongo miwili iliyopita, baada ya jumuiya ya awali kuvunjika mwaka 1977 kutokana na sababu mbalimbali.
Akieleza maono yake kwa EAC, Kenyatta alisema atazingatia kuimarisha ushirikiano ili kuongeza muunganiko wa ndani wa jumuiya na kuhakikisha utekelezaji endelevu wa miradi na mipango katika sekta za uzalishaji.
"Ni muhimu kwamba malengo ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Fedha na usafirishaji rahisi zaidi wa bidhaa, watu na huduma, unatimizwa," alisema.
Alisema ni hitaji muhimu la nchi washirika, kurahisisha mikakati iliyopo katika muingiliano huru wa watu, wafanyabiashara na huduma kama ilivyo katika itifaki ya pamoja.
Mkutano huo ulioongozwa na Rais Kenyatta, pia ulifanya uteuzi wa majaji wapya sita wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati akimkabidhi uenyekiti Rais Kenyatta, Rais Kagame alimpongeza kwa kuwa mwenyekiti mpya wa EAC.