Kenya imetuma kikosi maalum cha polisi kudhibiti mapigano ya kijamii yanayozidi kuongezeka katika mji wa Sondu, magharibi mwa mpaka wa Kericho-Kisumu.
Watu saba wamefariki na wengine kadhaa kuhama makazi yao katika mapigano mapya yaliyoanza siku ya Jumatano.
Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema kuwa wakuu wa usalama wa mashinani kutoka kaunti zote mbili za Kisumu na Kericho watahamishwa kufuatia makabiliano hayo.
"Maisha ya watu yamepotea, mali kuharibiwa na hali ya raia imedhoofishwa sana katika muda wa siku mbili zilizopita," Bw Kindiki alisema.
Viongozi wa eneo hilo wametaka kutatuliwa kwa haraka kwa mzozo wa mpaka kati ya jamii zinazozozana.
Watu watatu waliuawa katika mashambulizi kama hayo mwezi Julai.
Mji wa Sondu una historia ya ghasia mbaya za kikabila wakati wa chaguzi.