William Ruto amewataka viongozi wa dunia kuunga mkono wito wake wa marekebisho ya mifumo ya kifedha duniani
Rais wa Kenya William Ruto ameitaka Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupunguza hatua kali za mikopo zilizotolewa kwa nchi za Kiafrika ili kuhakikisha upatikanaji wa haki wa rasilimali.
"Afrika haitaki chochote bure. Lakini tunahitaji mtindo mpya wa kifedha ambapo mamlaka hayako mikononi mwa wachache," Bw Ruto alisema.
Ruto,ambaye alizungumza alipokutana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, mkuu wa IMF Kristalina Georgieva, na rais wa Kundi la Benki ya Dunia Ajay Banga mjini Paris Alhamisi, aliwataka viongozi wa dunia wanaohudhuria Mkutano wa New Global Financial Pact Summit kuunga mkono wito wake.
Utawala wa Bw Ruto ulipokea $600m (£470m) kutoka kwa IMF katika msimu wa vuli na baridi ya 2022.
Pia ulipata $993m kutoka Benki ya Dunia mwezi Mei kusaidia serikali kufadhili bajeti.
Nchi nyingi za Kiafrika zinakabiliwa na deni kubwa la nje ya nchi kutokana na mfumuko wa bei na kuongezeka kwa ukopaji.