Waziri wa elimu wa Kenya Ezekiel Machogu amepiga marufuku masomo yanayotolewa alfajiri na usiku katika shule mbali mbali "hatutaki kuwalazimisha watoto kuhangaika – watoto wanapaswa kulala masaa tisa ".
Bw Machogu ameagiza kuwa masomo yote katika shule za kibinafsi na za umma yatolewe kati ya saa mbili za asubuhi na saa tisa na dakila 45 alasiri ili kuhakikisha mafunzo yanatolewa katika muda uliopangwa.
"Mtaala unapaswa kukamilishwa katika muda uliopangwa. Tusiwaweke watoto katika hali ya mateso yasiyo muhimu," aliongeza.
Waziri huyo amesema ameshuhudia mtindo ambapo basi za shule huwachukua watoto kutoka nyumbani saa kumi na moja alfajiri na kuwarejesha kutoka shuleni saa mbili za usiku.
Suala la muda wanaoripoti shuleni wa wanafunzi limekuwa likiendelea kuibua mjadala nchini Kenya.
BBC ilifanya uchunguzi mwaka 2021 wakati kulipokuwa na ongezeko la juu la visa vya moto katika shule za malazi, na ilifichuliwa kwamba wanafunzi walikuwa wakianza masomo 04.30 hadi saa nne usiku .
Wanafunzi waliohojiwa wakati huo walilalamikia mpango wa muda mrefu wa masomo ya siku na ukosefu wa muda shughuli za nje ya masomo.