Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kenya yapeleka wanajeshi 200 kulinda amani DRC

Kenya Wanajeshi DRC Kenya yapeleka wanajeshi 200 kulinda amani DRC

Wed, 24 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kenya imepeleka zaidi ya wanajeshi wake 200 kushiriki katika opereseheni za kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo chini ya mwavuli wa kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa maarufu kwa jina la MONUSCO.

Wanajeshi hao waliagwa na Naibu Mkuu wa Majeshi ya Kenya Luteni Jenerali Francis Ogolla ambaye ametoa amri wanajeshi hao wafanye kazi zao kwa bidii, wachunge nidhamu na wabebe ujumbe wa amani na usalama wa taifa la Kenya.

Kwa miaka kadhaa sasa Kenya imekuwa na siasa za kupeleka wanajeshi wake kushiriki kwenye operesheni mbalimbali za kulinda amani. Luteni Jenerali Ogolla amewaambia wanajeshi hao kwamba, mtakapokuwa huko DRC, ni wajibu wenu kulinda heshima ya Kenya kwani huko hamuwakilishi tu jeshi la KDF bali mnalinda heshima ya nchi nzima.

Hayo yamekuja katika hali ambayo kwa muda mrefu sasa, wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekuwa wakilalamikia utendaji mbovu wa kikosi hicho. Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai, wananchi hao waliyashambulia makao makuu ya MONUSCO katika mji wa Goma, ambao ni makao makuu ya mkoa uliogubikwa na machafuko wa Kivu Kaskazini na ambao unapakana na Rwanda na Uganda.

Wakazi wa mji wa Goma walisema kuwa, ujumbe wa MONUSCO unapaswa kuondoka nchini humo haraka iwezekanavyo, kwani uwepo wake haujasaidia chochote katika kurejesha usalama na utulivu nchini humo.

Mamia ya wakazi wa mkoa huo walifunga barabara zote muhimu za mji huo kabla ya kuandamana hadi makao makuu ya kikosi cha MONUSCO, wakitaka kuondoka askari hao wa kulinda amani, kutokana na kile wanachodai kuwa, ni uzembe katika utendaji wao wa kazi kwa zaidi ya miongo miwili tangu watumwe nchini humo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live