Rais wa Kenya William Ruto anasema alikataa ombi la kukamatwa kwa wanasiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walioanzisha muungano na waasi mjini Nairobi siku ya Ijumaa.
Corneille Nangaa, mkuu wa zamani wa baraza la uchaguzi la DR Congo, Ijumaa alitangaza katika hoteli moja katika mji mkuu wa Kenya kwamba anaunda muungano wa kisiasa na kijeshi na waasi wa M23 na makundi mengine yenye silaha kwa lengo la kurejesha amani.
Bw Nangaa alikuwa pamoja na kiongozi wa M23 Bertrand Bisimwa.
Hatua hiyo iliibua jibu la hasira kutoka kwa serikali ya Kongo ambayo ilionya Kenya kuhusu "matokeo" ya kumkaribisha.
Rais Ruto, ambaye alizungumza na wanahabari wa Kenya katika mahojiano siku ya Jumapili, alisema alikataa kutii ombi la kuwakamata wanasiasa hao wa DR Congo, na kulitaja kuwa "lisilo la kidemokrasia."
"Kenya ni demokrasia. Hatuwezi kumkamata yeyote ambaye ametoa taarifa. Hatuwakamati watu kwa kutoa matamshi, tunawakamata wahalifu," Bw Ruto aliongeza.
Siku ya Jumamosi, serikali ya Kongo ilimwita balozi wa Kenya mjini Kinshasa na pia kumrudisha nyumbani balozi wake Nairobi kwa "mashauriano".
Akijibu, Bw Ruto alisema ni haki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya hivyo, "Lakini siwezi kumkamata mtu yeyote kwa sababu tu walitoa taarifa. Hiyo ni kinyume cha demokrasia, na sivyo Kenya ilivyo."
Wizara ya mambo ya nje ya Kenya hapo awali ilisema "inajitenga vikali" na masuala ya ndani ya DR Congo, na kuongeza kuwa imeanza kuchunguza suala hilo.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inajiandaa kwa uchaguzi utakaofanyika siku ya Jumatano huku hali ya ukosefu wa usalama ikizidi kuwa mbaya katika eneo la mashariki, ambako zaidi ya makundi 100 yenye silaha, ikiwa ni pamoja na M23, yanaendesha harakati zake.