Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kenya yagundua hifadhi za madini ya coltan

Madini Ya Coltan Kenya yagundua hifadhi za madini ya coltan

Thu, 25 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kenya imegundua mabaki yake ya kwanza ya madini ya coltan yenye thamani, waziri wa madini amesema.

Madini hayo adimu hutumika kutengeneza betri za magari ya umeme, simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inashikilia zaidi ya 70% ya hifadhi ya coltan duniani, ambayo kwa miongo kadhaa imechochea mapigano makali mashariki mwa nchi.

Haijabainika ni nyingi kiasi gani mabaki hayo ya coltan yaliyopatikana nchini Kenya.

Maafisa wa uchimbaji madini hapo awali walidokeza kwamba Kenya inaweza kuwa na chembechembe za madini hayo yenye thamani kubwa, lakini Waziri wa Madini, Uchumi wa Bluu na Masuala ya Bahari wa Kenya Salim Mvurya Jumatano alisema kuwa tangazo lake linamaanisha "sasa ni rasmi" kwamba Kenya ina hifadhi ya coltan.

Hifadhi za madini hayo zimepatikana katika kaunti sita kote nchini, lakini thamani yake bado haijabainika.

"Tutaziacha timu zetu ziendelee na utafiti wao ili sasa tuanze kutathmini thamani ya kiuchumi ya madini hayo," Bw Mvurya alisema.

Wakaazi wa Kaunti ya Embu mashariki mwa Kenya, mojawapo ya kaunti sita zilizo na hifadhi ya madini hayo, wameshauriwa kushikilia ardhi zao.

"Madini ya thamani yamepatikana hapa na ikiwa unataka kufaidika usiuze ardhi yako," Nebart Muriuki, mbunge kutoka kaunti hiyo, alinukuliwa akizungumza na gazeti la kibinafsi la Afrika Mashariki.

Bw Mvurya alisema ugunduzi huo unatarajiwa kubuni nafasi zaidi za kazi na kupanua sekta ya madini nchini Kenya, ambayo ilichangia shilingi bilioni 120.3 za Kenya ($735m; $577m) kwa uchumi wa nchi hiyo mwaka wa 2022.

Coltan mara nyingi husafishwa kuwa metali tantali, poda inayostahimili joto ambayo hutumiwa kutengeneza vidhibiti, ambavyo hutumika kutengeneza vifaa vya kielektroniki.

Bei ya coltan inategemea ni kiasi gani cha tantali iliyomo, lakini kwa wastani, kilo moja ya madini hayo adimu inafikia $48 (£37), kulingana na Forbes.

Wachambuzi wanasema mahitaji ya kimataifa ya coltan yanakua kwa kasi na imekuwa mojawapo ya vichochezi vinavyochochea vita mashariki mwa DR Congo, huku wanamgambo hasimu wakipigania udhibiti wa migodi inayozalisha coltan na madini mengine ya thamani.

DR Congo, pamoja na nchi jirani ya Rwanda, ni wasambazaji wakuu wa coltan duniani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live