Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kenya yaahidi kupeleka maafisa wengine 600 wa polisi nchini Haiti

Polisi Wengine 200 Wa Kenya Waelekea Haiti.png Kenya yaahidi kupeleka maafisa wengine 600 wa polisi nchini Haiti

Fri, 11 Oct 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Kenya William Ruto ametangaza siku ya Ijumaa Oktoba 11, 2024 kwamba maafisa 600 wa ziada wa polisi watatumwa kwa misheni ya kimataifa ya usaidizi wa usalama nchini Haiti, wakati Waziri Mkuu wa nchi hii iliyoharibiwa na vita vya magenge alipokuwa ziarani nchini Kenya.

Kenya ilianza kupeleka wanajeshi wake wa kwanza nchini Haiti msimu huu wa joto, ambao sasa wana idadi ya chini ya maafisa wa polisi 400, pamoja na takriban maafisa zaidi ya ishirini wa polisi kutoka Jamaica na Belize.

"Ninafuraha kutangaza kwamba maafisa wengine 600 wa polisi wa Kenya wanamaliza mafunzo yao kabla ya kutumwa na watakuwa tayari kuanza majukumu yao mwezi ujao," Ruto amesema katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu wa Haiti, Garry.

Bw Ruto, ambaye alitoa hakikisho mwishoni mwa mwezi wa Septemba kwamba nchi yake itakamilisha kutumwa kwa maafisa 2,500 wa polisi kufikia mwezi Januari 2025, hakubainisha ni lini maafisa hao 600 wa ziada wa polisi watatumwa. Rais wa Kenya pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa "haraka" kuunga mkono misheni hii ambayo inakabiliwa na ukosefu wa fedha na vifaa.

"Tungependa kuona jibu la haraka, tungependa kuona kujitolea zaidi na tutaendelea kuweka shinikizo katika mwelekeo huu," ameongeza Bw. Conille. Waziri Mkuu huyo wa muda alizuru Kenya wiki moja baada ya shambulizi kali la genge lililoua watu 109 na kuwajeruhi zaidi ya arobaini.

Wanachama wa genge lililojihami kwa silaha waliwafyatulia risasi wakaazi katika mji wa Pont-Sondé, ulioko takriban kilomita 100 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu Port-au-Prince, wakiteketeza makumi ya nyumba na magari. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliongeza muda wa ujumbe wa polisi wa kimataifa kwa mwaka mwingine mwezi uliopita, bila kutaja uwezekano wa kubadilishwa kwake kuwa kikosi cha Umoja wa Mataifa kama ilivyoombwa na mamlaka mpya ya nchi hiyo.

Haiti imeteseka kwa muda mrefu kutokana na ghasia za makundi hayo yenye silaha, ambayo yanadhibiti asilimia 80 ya mji mkuu wa Port-au-Prince na barabara kuu za nchi hiyo. Takriban watu 3,661 wameuawa tangu mwezi wa Januari nchini Haiti, iliyoathiriwa na ghasia, kulingana na takwimu iliyotajwa mwishoni mwa mwezi wa Septemba na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu.

Wimbi la ghasia na hali mbaya ya kibinadamu imewalazimu zaidi ya watu 700,000, nusu yao wakiwa watoto, kukimbia makazi yao na kutafuta hifadhi kwingineko nchini humo, kwa mujibu wa takwimu za hivi punde za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live