Madereva wa magari mjini Namanga katika mpaka wa Tanzania na Kenya sasa wamegeukia kununua mafuta katika taifa jirani la Tanzania huku bei ghali za bidhaa hiyo zikishika kasi kote nchini.
Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli nchini Kenya (EPRA) mnamo Ijumaa iliongeza bei ya lita moja ya petroli kwa Sh17 hadi kufikia Sh211.64, dizeli kwa Sh21 hadi kufikia Sh200.99, mafuta taa kwa Sh33 hadi Sh202.61 jijini Nairobi na viungani mwake.
Udadisi uliofanywa jana na Taifa Dijitali ulifichua kuwa lita moja ya petroli inauzwa kwa Sh184.18 huku dizeli ikiuzwa kwa Sh186.76.
Kwa kununua bidhaa hiyo nchini Tanzania, waendeshaji wa magari Wakenya wanaokoa jumla ya Sh27.46 kwa kila lita moja ya petroli na Sh14.23 kwa dizeli.
Magari na pikipiki za Kenya jana zilifurika katika Kituo cha Petroli cha Admire, umbali wa kilomita moja kutoka mpakani.
Mhudumu aliyezungumza na Taifa Dijitali alisema mauzo yamepanda katika muda wa siku mbili zilizopita. “Biashara kwetu imenoga,hatulalamiki,” alisema.
Kwingineko, waendeshaji bodaboda nchini wanakabiliwa na hali ngumu kufuatia kuongezwa kwa bei za mafuta huku abiria wengi wakiamua kutembea kwa miguu katika masafa mafupi badala ya kulipa nauli ya juu.
Willis Jillo ni mfano wa waendeshaji pikipiki wengi wanaohofia kupokonywa pikipiki zao walizonunua kwa mikopo baada ya kushindwa kulipia kiasi cha kila siku.
Bw Jillo anayehitajika kulipa Sh300 kila siku kwa shirika lililomkopesha, ameshindwa kufanya hivyo kwa siku tatu baada ya bei ghali za mafuta kuvuruga biashara.
“Walinipigia simu jana jioni wakiniagiza kuhakikisha sina deni lolote kufikia mwisho wa leo la sivyo wakakujia pikipiki jioni kwa hivyo nina hadi saa tisa adhuhuri,” alisema.
“Tumekuwa tukilipisha abiria wetu Sh50 kwa masafa ya chini ya kilomita mbili lakini ni hapo mbeleni wakati bei za mafuta zilikuwa afadhali. Tumejitahidi kudumisha kiwango hicho hata baada ya bei kuongezwa zaidi japo hatukuwa tunapata faida yoyote. Bei hiyo haiwezi ikatumika sasa.”
Katika eneo la Pwani, watalii na wageni wanaozuru nchini hasa Kisiwa cha Lamu tayari wameanza kuhisi ugumu wa gharama ya juu ya maisha kutokana na ongezeko la bei ya mafuta.
Hii ni baada ya kuongezeka kwa bei ya mapochopocho, hasa yale ya samaki hotelini na mikahawani eneo hilo.
Kwa kawaida, bakuli la mlo wa samaki katika hoteli za kifahari Kisiwani Lamu huuzwa kwa kati ya Sh3,000 na Sh3,500.
Katika hoteli na mikahawa ya kawaida, sinia ya mlo wa samaki huuzwa kienyeji kwa kati ya Sh700 na Sh1500.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Dijitali mwishoni mwa juma ulibaini kuwa tangu nyongeza ya mafuta kutangazwa na serikali wiki jana, wenye hoteli na mikahawa kisiwani Lamu na viungani mwake wamelazimika kuongeza bei ya vyakula, hasa vile vya baharini kutokana na kwamba wamiliki hao wa mahoteli wamekuwa wakinunua bidhaa ya samaki kutoka kwa wavuvi kwa bei ghali.
Baadhi ya wavuvi waliozungumza na Taifa Dijitali walisema wamelazimika kusitisha shughuli baharini na kuegesha vyombo vyao, ikiwemo mashua, jahazi na boti za uvuvi maskani kwani hawawezi kukimu gharama ya juu ya mafuta kusafiri baharini kuvua.