Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kenya nchi ya kwanza Afrika kutembelewa na Rais wa Iran

Iran Kenya Safari Mara Ya Kwanza Kenya nchi ya kwanza Afrika kutembelewa na Rais wa Iran

Wed, 12 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema leo Jumatano amewasili Nairobi mji mkuu wa Kenya akiongoza ujumbe wa ngazi za juu, akiwa katika ziara ya kuzitembelea nchi tatu za Kenya, Uganda na Zimbabwe.

Kenya ni kituo cha kwanza katika safari ya Sayyid Ebrahim Raisi barani Afrika; na baadaye atalekea Uganda na Zimbabwe. Hii ni ziara ya kwanza ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran barani Afrika baada ya miaka 11.

Jana usiku na kabla ya kuanza safari ya kuelekea Nairobi, Rais Ebrahim Raisi alisema katika Uwanja wa Ndege wa Mehrabad mjini Tehran kwamba lengo la safari yake ya kuzitembelea nchi hizo tatu ni "kuitikia mwaliko rasmi wa marais wa nchi hizo na kuimarisha ushirikiano, akisisitiza kuwa bara la Afrika linapewa umuhimu mkubwa katika siasa za mambo ya nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Muda mchache baada ya kuwasili, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Rais amepokewa rasmi na mwenyeji wake, Rais William Ruto wa Kenya katika Ikulu ya Nairobi na amepigiwa mizinga 21 kwa heshima yake.

Mara baada ya hafla ya kukaribishwa rasmi, marais wa Iran na Kenya walifanya mazungumzo ya faragha na baadaye kumetiwa saini hati tano muhimu za ushirikiano wa pande mbili mbele ya marais hao wawili. Hati hizo zinahusiana na sekta za mawasiliano, uvuvi, kilimo, afya na elimu ya ufundi, maarifa na matibabu.

angu iliposhika hatamu za uongozi Agosti 2021 Serikali ya Awamu ya 13 ya Iran ilianzisha juhudi kubwa za kulipa kipaumbele maalumu suala la uwezo na fursa zilizopuuzwa na kusahaulika duniani na kutumika suala hilo kadiri inavyowezekana katika kupunguza vikwazo vya kiuchumi na kubatilisha njama za kutaka kuitenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kisiasa na kiuchumi. Nchi jirani za Eurasia, Amerika ya Kusini na sasa Afrika zina uwezo na fursa hizo, na uwepo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kila moja kati ya kanda hizi kunaweza kutambuliwa kama sehemu ya mipango ya serikali ya Iran katika uwanja wa kuvutia uwekezaji wa kigeni na pia kutayarisha mazingira mwafaka ya uwepo imara zaidi katika maeneo hayo.

Kenya inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi muhimu za Afrika Mashariki na lango la kuingia katika bara hilo; hivyo basi, kupanuliwa uhusiano na nchi hii katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kisayansi na kiteknolojia kutakuwa sababu ya kuzidisha satua na ushawishi wa Iran katika nchi hiyo na eneo zima la Mashariki mwa bara la Afrika.

Uhusiano kati ya Iran na Kenya ulianza mwaka 1971. Uhusiano huo ulikatwa mwaka 1977 baada ya uhasama na mapigano baina ya Ethiopia na Somalia wakati utawala wa kifalme wa Iran ya wakati huo ulipowaunga mkono waasi wa Somalia. Tehran na Nairobi zilianzisha tena uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1982 baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyofanyika mwaka 1979.

Japokuwa kumekuwepo safari za maafisa wa Iran na Kenya katika nchi hizo mbili tangu wakati huo lakini kivitendo, hakushuhudiwi msukumo mkubwa katika uhusiano wa kiuchumi; na sababu kuu na hali hiyo ni kwamba Kenya imekuwa chini ya mashinikizo yanayoitaka isianzishe uhusiano wowote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mnamo 2013, baada ya duru kadhaa za mazungumzo na maafisa wa Kenya, kulifanyika jitihada za kubadilisha hali ya ubaridi iliyotawala uhusiano wa nchi hizo mbili. Tangu wakati huo, Kenya imekuwa na uhusiano mzuri na Iran, na wakati fulani tulishuhudia usafirishaji wa tani milioni 4 za mafuta nchini humo kutoka Iran na kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja za ndege kati ya Tehran na Nairobi.

Kulingana na takwimu rasmi, kiwango cha biashara kati ya Iran na Kenya ni takriban dola milioni 100 kwa mwaka, ingawa takwimu zisizo rasmi zinaonyesha idadi kubwa kuliko hii. Kwa mfano, usafirishaji wa "lami" pekee kutoka Iran hadi Kenya unakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 50. Bidhaa muhimu zaidi za Kenya zinazouzwa Iran ni pamoja na malighafi ya madini, chai na kahawa; na bidhaa muhimu zaidi zinazoagizwa na Kenya kutoka nje ni lami, chakula na mada za kemikali.

Kenya ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kiasi barani Afrika, na kwa upande wa usafiri wa baharini, inaweza kuwa moja ya washirika wazuri wa Iran na kiunganishi kati ya Iran na nchi za mashariki na katikati mwa Afrika.

Kenya pia ina nia ya kutumia njia za usafirishaji za Iran kufika Ulaya na Asia. Vilevile itakuwa soko zuri la bidhaa za viwandani za Irani; na kutokana na kuwa na vyanzo vya maji na ardhi yenye rutuba, inaweza kuwa mojawapo ya malengo ya Iran kwa ajili ya kilimo nje ya nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live