Kenya na Umoja wa Ulaya, zimetia saini mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi, maarufu kama EPA.
Mkataba huo, umetiwa saini jijini Nairobi, mbele ya rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von Der Leyen na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairob hapo jana.
Mkataba huo unaeleza kuwa Kenya itafungua soko lake kwa bidhaa kutoka Ulaya hatua kwa hatua.
“Hatua hii ni tangazo kwa dunia kuwa Kenya iko tayari kuzalisha bidhaa zenye viwango vya juu kwenda kwenye soko la Ulaya, ” amesema rais Ruto na kuongeza kuwa Kenya itasafirisha bidhaa zilizokamilika na sio malighafi.
Kwa upande wake Ursula von Der Leyen Mkuu wa Tume ya Umoja wa Ulaya amesema, hatua hiyo inaimarisha zaidi ushirikiano kati ya Kenya na Ulaya.
“Umoja wa Ulaya, unathamini sana ushirikiano huu. Soko la Ulaya litafunguliwa kwa bidhaa kutoka Kenya,” amesema Ursula akiongeza kuwa mkataba huo uko wazi kwa nchi nyingine za kikanda. Rais William Ruto akiwa katika mazungumzo na Ursula von Der Leyen Mkuu wa Tume ya Umoja wa Ulaya
Baada ya kutiwa saini, watalaamu kutoka Kenya na Umoja wa Ulaya watakutana kila baada ya miaka mitano kuuthathmini mkataba huo.
Kwa mujibu wa mkataba huo, bidhaa zinazotoka Kenya kwenda kwenye soko la nchi za Umoja wa Ulaya, hazitatozwa kodi.
Miongoni mwa bidhaa ambazo Kenya inatarajiwa kuuza kwenye soko la Ulaya ni pamoja na maua, chai, kahawa, nyama na ngozi, mbogamboga na matunda miongoni mwa bidhaa nyingine, huku Ulaya ikiingiza bidhaa za viwandani kama dawa na kemikali.
Kenya imekuwa nchi ya kwanza kuingia kwenye mkataba huo wa EPA, ambao awali ulikuwa uyashirikishe mataifa yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkataba huo, ulikuwa utekelezwe kuanzia mwaka 2014 lakini Kenya na Rwanda ndizo zilizokuwa tayari, na kuilazimu Brussels kuubadilisha ili kushirikiana na nchi moja moja kwenye jumuiya ya EAC.
Baada ya kutiwa saini, mkataba huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Machi mwaka ujao, baada ya bunge la Kenya na lile la Umoja wa Ulaya kuupitisha mswada huo mwezi Februari Tanzania na Uganda zinataka mkataba huo kufanyiwa mabadiliko zaidi kabla ya kuukubali