Serikali za Kenya na Norway zinaongoza mazungumzo kati ya serikali ya Ethiopia na waasi wa Oromo Liberation Army (OLA), vyanzo vilivyo karibu na mazungumzo hayo vimeiambia BBC.
Marekani, Umoja wa Ulaya na Sweden zinaunga mkono mazungumzo yaliyoanza siku tatu zilizopita huko Zanzibar, Tanzania.
Duru hizo zilisema kuwa pande hizo mbili zilikuwa zikiandaa ajenda za mazungumzo hayo ya amani lakini hazikutoa maelezo zaidi.
Ujumbe wa serikali kwa mazungumzo ya amani unaongozwa na mshauri wa usalama wa kitaifa wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed, Balozi Redwan Hussein, na Waziri wa Sheria Gedion Temoteos.
Wawili hao pia walikuwa sehemu ya mazungumzo ya amani kati ya serikali na viongozi wa eneo la Tigray, ambayo yalimaliza mzozo wa miaka miwili eneo la kaskazini.
OLA inawakilishwa na mwanahistoria kutoka Marekani Prof Mohammed Hassan, mshauri mkuu wa kamanda wa OLA, Jirenya Gudeta.
Mazungumzo yalitarajiwa kukamilika kufikia Jumapili, lakini vyanzo viliiambia BBC kwamba mazungumzo hayo yanaweza kuendelea kwa muda mrefu zaidi.
Kundi la OLA limekuwa likipambana na vikosi vya serikali tangu lilipojitenga na kundi la waasi mwaka 2018.
Mazungumzo hayo yanakuja takriban miezi sita baada ya serikali ya Ethiopia kufikia makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya miaka miwili vya umwagaji damu huko Tigray.