Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Alfred Mutua amesema nchi yake iko tayari kuongoza kikosi cha kimataifa nchini Haiti; na itapeleka maafisa 1,000 wa polisi katika taifa hilo la Karibean lililokumbwa na mapigano mara tu pendekezo lake litakapokubaliwa.
Mutua ameongeza kuwa, ahadi inayotoa Kenya ni kupeleka kikosi cha askari polisi 1,000 kusaidia kutoa mafunzo na kusaidia polisi wa Haiti ili kurejesha hali ya kawaida nchini humo na kulinda mitambo ya kimkakati.
Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Kenya, mpango huo iliopendekeza unahitaji kwanza idhini ya mamlaka kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ridhaa ya mamlaka ya ndani nchini Haiti.
Kwa karibu mwaka mmoja sasa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry wamekuwa wakitoa wito wa kuchukuliwa hatua za uingiliaji kati kimataifa nchini Haiti ili kuisaidia polisi ya nchi hiyo, lakini hadi sasa hakuna nchi iliyojitokeza na kuonyesha utayari wa kuongoza juhudi hizo. Hali ya mchafukoge Haiti
Mapema mwezi huu Guterres alisema, ghasia zimeendelea kuongezeka na kuenea nchini Haiti, akiashiria matukio ya mauaji, utekaji nyara, ubakaji wa wanawake na wasichana, uporaji, na kwa maelfu ya watu kuhama makazi yao.
Hivi sasa magenge mbalimbali yanadhibiti karibu asilimia 80 ya mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince huku uhalifu wa kikatili kama vile utekaji nyara kwa ajili ya kulipwa kikomboleo, wizi wa kutumia silaha na utekaji nyara wa magari vikiwa ni mambo ya kawaida nchini humo.