Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kenya kuomba mkopo wa ziada wa $1bn kutoka China

Kenya Kuomba Mkopo Wa Ziada Wa $1bn Kutoka China Kenya kuomba mkopo wa ziada wa $1bn kutoka China

Fri, 6 Oct 2023 Chanzo: Bbc

Rais wa Kenya William Ruto atasafiri kuelekea Uchina baadaye mwezi huu kutafuta mkopo wa $1bn (£820m) kulipia miradi iliyokwama ya barabara, naibu wake Rigathi Gachagua amesema.

Bw Gachagua aliambia redio ya Inooro FM inayotangaza kwa lugha ya kienyeji kwamba wanakandarasi wengi wameacha miradi kote nchini kwa vile hawakulipwa kwa kazi yao.

Alisema wakati Kenya tayari ina deni kubwa kwa Uchina, rais ataomba nyongeza ya $1bn huku akiomba muda mrefu zaidi wa kulipa pesa ambazo tayari zinadaiwa.

Alisema rais atawaambia Wachina kwamba "tunakubali kwamba tunadaiwa pesa, tunaweza kuzungumza ili muongeze muda zaidi, tulipe polepole zaidi, na je munaweza kuongeza pesa kidogo ili kumaliza ujenzi wa barabara zetu?".

Kenya inadaiwa na China zaidi ya $8bn kutokana na mikopo ambayo mara nyingi ilitolewa wakati wa uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Naibu rais alizungumzia swala la ubadhirifu unaofanywa na maafisa wa serikali akisema hiyo ndiyo sababu rais aliagiza kuzuiliwa kwa safari za nje.

Mapema wiki hii, ofisi ya rais ilipiga marufuku maafisa wa umma kuchukua safari zisizo za lazima nje ya nchi ili kubana matumizi na ameziagiza wizara zote kupunguza bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa asilimia 10.

Serikali imeshutumiwa kwa matumizi yasiyo ya lazima huku kukiwa na malalamiko ya Wakenya wengi kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha na nyongeza ya ushuru iliyowekwa na serikali.

Chanzo: Bbc