Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kenya kufungua shule za msingi na upili 2021

KENYA SHULE Kenya kufungua shule za msingi na upili 2021

Tue, 7 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Elimu nchini Kenya imetangaza kuwa shule za msingi na upili zitafunguliwa mwaka 2021.

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amesama mitihani ya kitaifa sasa haitafanyika mwaka huu kutokana na athari iliyosababishwa na janga la corona.

''Tulikuwa tumepanga wanafunzi wa darasa la nane na kidato cha pili warudi shuleni lakini tumebadili wazo hilo'' aliongeza Bw. Magoha.

Waziri Magoha amesema uamuzi huo ulifikiwa kufuatia majadiliano ya kina yaliojumuisha washikadau wote katika sekta ya elimu.

''Shule zitafunguliwa endapo idadi ya maambukizi kwa siku itapungua kwa siku 14 mfululizo''

Vyuo vikuu na vitafunguliwa kwa awamu lakini wasimamizi wametakiwa kuzingatia muongozo wa kinga uliotolewa na wizara ya Afya.

''Vyuo ambavyo vitakiuka muongozo huo vitafungwa'' alisema Bw. Magoha katika hotuba yake kwa taifa.

Siku ya Jumanne Rais Uhuru Kenyatta aliondoa masharti ya usafiri wa kuingia na kutoka katika miji ya Nairobi, Mombasa na Mandera kaskazini mwa nchi.

Rais Kenya hata hivyo aliwatahadharisha kutolegeza juhudi za kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 akiongeza kuwa ni juhudi ya mtu binafsi.

Licha ya kuondolewa kwa marufuku ya usafiri Wakenya bado wametakiwa kuzingatia kafyu ya kitaifa ya kutotoka nje kati ya saa kumi tatu usiku na saa kumi alfajiri.

Safari za ndani na nje ya Kenya

Siku ya Jumanne Rais Kenyatta pia alitangaza kuwa safari za ndege ndani ya Kenya zitaanza tena tarehe 15 mwezi Julai mwaka 2020, kwa kuzingatia miongozo na kanuni kutoka kwa wataalamu wa afya kutoka wizara ya afya na mamlaka ya usafi wa anga nchini humo.

Safari za kimataifa za kuingia na kutoka nchini zitaanza tarehe 1 mwezi Agosti 2020.

Wanasayansi nchini Kenya wanakadiria kwamba huenda Wakenya milioni 2.6 tayari wana virusi vya corona, hayo yamejitokeza baada ya wanasayansi kupima damu iliyotolewa kwa ajili ya protini inayotumika kwenye mfumo wa kinga.

Kwa mujibu wa data ya utafiti wa Taasisi ya Matibabu Kenya pamoja na Tasisi ya Afya ya Wellcome Trust, takriban watu 550,000 sawa na asilimia 12. 4 ya wakazi wa Nairobi kati ya raia milioni 4.4 tayari walikuwa wamejenga kinga ya mwili kabla ya kutangazwa kwa mgonjwa wa kwanza wa Covid-19 nchini humo Machi 13.

Katibu mkuu wa chama cha madaktari nchini Kenya (KMPDU) daktari Chibanzi Mwachonda anaonya kuwa hali ya huduma hospitalini ni tete.

''Kumekuwa na ongezeko la maambukizi katika mwezi wa Juni na Julai lakini pia kumekuwa na shinikizo kutoka wa wananchi la kufunguliwa tena kwa shughuli za kiuchumi.''

Kulingana na daktari Mwachonda huenda kipindi hiki ambapo masharti yamelegezwa kikawa muhimu katika kujua kama kweli Kenya iko tayari kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona kikamilifu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live