Mdhibiti wa mawasiliano nchini Kenya amesema kuwa nchi hiyo ilikumbwa na rekodi ya mashambulizi ya mtandaoni milioni 860 katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Amesema kuwa "masafa, ustaarabu na ukubwa wa vitisho vya mtandao" vinavyolengwa katika miundombinu muhimu ya habari nchini Kenya vimeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Mnamo 2017, Kenya ilikumbwa na mashambulio ya mtandao milioni 7.7.
Mnamo Julai, shambulio la mtandaoni lililohusishwa na kundi linalounga mkono Urusi la udukuzi la Anonymous Sudan lilizuia ufikiwaji wa zaidi ya huduma 5,000 za serikali za mtandaoni nchini humo, yakiwemo maombi ya viza, pasipoti na leseni ya udereva.
Shambulio hilo pia lilizima mifumo ya kuhifadhi nafasi za treni mtandaoni na miamala ya pesa ya simu ya mkononi.
Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya Jumatatu ilisema kuwa 79% ya mashambulizi yaliyorekodiwa katika miezi 12 iliyopita yalisababishwa na wahalifu wa mtandao kujipenyeza kwenye mifumo ya kompyuta ya mashirika.
Mdhibiti huyo pia alisema kuwa 14% ya mashambulizi yalihusisha programu hasidi, 6.5% ilihusisha wahalifu wa mtandao waliojaza seva, mawasiliano gushi ili kupakia miundombinu yao na mashambulio yaliyosalia yalilenga programu za wavuti.
Kulingana na mdhibiti huyo, Kenya sasa ni nchi ya tatu inayolengwa zaidi na wahalifu wa mtandao barani Afrika, baada ya Nigeria na Afrika Kusini.