Maeneo mbalimbali nchini Kenya yanakabiliwa na mafuriko wakati huu mvua kubwa ikiendelea kunyesha kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.
Kaunti ya Mombasa pwani ya taifa hilo na Tana River huko kaskazini Mashariki ni baadhi ya majimbo yalioathirika.
Shirika la msalaba mwekundu nchini humo limesema familia 156 huko Bandi, Garsen katika Kaunti ya Tana River hawana makazi na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka huku watu wengi wakitafuta maeneo ya juu.
Zaidi ya watoto 20 na mama zao wamesafirishwa hadi kambi mpya iliyoanzishwa karibu na mji wa Garsen.
Kwa mujibu wa baadhi ya video zilizosambazwa na shirika hilo la vyombo vya habari vya ndani, baadhi ya makaazi ya watu yamejaa maji haswa katika kaunti ya Mombasa.
Ripoti kutoka kwa shirika la msalaba mwekundu zinaeleza kuwa watu 52 wamefariki kutokana na mafuriko wakati huu wengine 24,415 wakiwa wamepoteza makazi yao katika maeneo tofauti ya nchi.
Mkoa wa bonde la ufa umeripoti vifo vya watu 15 wengine watatu wakipata majeraha madogo, 1,657 wakiyahama makazi yao kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa inayoendelea.
Katika eneo la Nyanza, watu sita wameripotiwa kufariki, wengine 116 wakipoteza makazi yao.