Wahifadhi wa mazingira nchini Kenya wanaomboleza kifo cha tembo mwenye umri wa miaka 65 katika mbuga ya wanyama ya Tsavo Mashariki.
Tembo huyo ambaye alibatizwa jina la ‘Dida’ alikufa kwa sababu ya uzee, kulingana na Shirika la Huduma ya Wanyamapori la Kenya.
‘Dida’ anayejulikana pia kama ‘Malkia wa Tsavo’ alikuwa amenusurika na changamoto nyingi kama vile ukame na ujangili katika eneo kubwa zaidi la uhifadhi nchini Kenya.
Wanamazingira waliingia kwenye mtandao wa Twitter kumsifu ‘Dida’ wakimtaja kuwa mstahimilivu wakati wa dhiki.
Waliezeka picha zake alipokuwa akitembea kwenye mbuga kubwa zaidi ya wanyamapori nchini iliyofunikwa kwenye udongo mwekundu na pembe zake ndefu.
Wasimamizi wa mbuga hiyo walimtaja Dida kama kiongozi mashuhuri wa Tsavo.
Wakati huo huo, ndovu wawili wamekufa kwa njaa katika Msitu wa Imenti huko Mlima Kenya.
Ukame wa sasa umeathiri wanyamapori huku zaidi ya ndovu 100 wakiripotiwa kufa katika Mbuga za Kitaifa za Tsavo Mashariki na Magharibi huko Kusini-mashariki mwa Kenya, kulingana na Wakfu wa Wanyamapori wa Afrika nchini Kenya.