Kushindwa kwa serikali ya Kenya kuwalipa mishahara watumishi wa umma kunazorotesha utoaji huduma muhimu na uzalishaji, hali ambayo inasababisha athari zaidi za kiuchumi nchini humo.
Watumishi hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe, waliiambia Sauti ya Amerika kwa njia ya simu kuwa wanashindwa kutekeleza majukumu yao na badala yake wanajihusisha na shughuli nyingine kama vile kilimo na biashara ndogondogo ili waweze kukidhi mahitaji ya familia zao.
Wamesema wanapambana na hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na serikali kushindwa kuwalipa mishahara tangu mwezi Januari.
“Hapo awali mishahara ilikuwa haichelewi, tulikuwa tukipokea mapema kati ya tarehe 25 hadi 28 ya kila mwezi” alisema mtumishi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe akihofia kupoteza ajira.
“Ni tatizo kubwa” alisema mwalimu mmoja ambaye pia hakutaka jina lake litajwe, aliongeza kwa kusema katika shule anayofundisha walimu wameacha kuja kazini wakifanya shughuli mbalimbali za kujiajiri.
“Jana nilikuwa nikiongea na rafiki yangu ambaye ni mwalimu aliniambia hali ndiyo hivyo hivyo , tunajikaza , hata chakula ni tatizo” alisema.
“Walimu tumekuwa tukiishi kwa kukopa chakula na mahitaji mengine muhimu kutoka kwa wafanya biashara wadogo wadogo, kwa sasa kukopeshwa inakuwa vigumu, kwa kuwa hujalipa deli lililopita” aliongeza.
Katika mahojiano na Sauti ya Amerika, Mwana harakati wa haki za jamii Julius Okoth amesema changamoto za kiuchumi zimeongeza shauku na kuwafanya wananchi wengi kujitokeza katika maandamano yaliyoitishwa na kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga ambaye anaupinga utawala wa rais William Ruto.
Okoth alisema maandamano hayo ambayo yalikuwa yakifanyika katika maeneo mbali mbali nchini Kenya, yalipata kasi na kuungwa mkono na watu wengi pale Odinga alipoingiza agenda za kiuchumi akitaka kushuka kwa gharama ya maisha na kutaja ongezeko la bei za mahitaji muhimu kama vile unga wa mahindi.
“Alipoanzisha maandamano yalikuwa yamezorota, alikuwa akizungumzia suala la wizi wa kura, shauku ilikuwa ndogo alipobadilisha na kuanza kuzungumzia uchumi na ugumu wa maisha hapo ndipo tulipoanza kuona watu wanajitokeza” Alisema mwanaharakati hyo.