Maafisa wa upelelezi na wataalam wanaochunguza madhehebu ya maangamizi nchini Kenya wamefukua mwili wa mtu uliokuwa na alama zinazoashiria mateso aliyopitia kabla ya kufariki katika shamba kubwa linalohusishwa na ibada hiyo.
Mwili huo ulizikwa huku mikono ya marehemu ikiwa imefungwa mgongoni. Takriban watu 428 wanaoaminika kuwa wafuasi wa kanisa la Good News International wamekufa, wengi wao kutokana na njaa.
Serikali ya Kenya inapanga kuendelea na awamu ya tano ya uchimbaji wa miili katika msitu wa Shakahola mwezi ujao.
Mwanapatholojia mkuu wa serikali ya Kenya anatarajiwa kufanya uchunguzi wa maiti ili kubaini chanzo cha kifo.
Maafisa wa upelelezi wanaamini kuwa marehemu ni mmoja wa watu wanaoshukiwa kuwa wasaidizi wa kiongozi wa kidini Paul Mackenzie.
Askari wa Jeshi la Ulinzi la Kenya, ambao wanashiriki katika operesheni ya uokoaji wanasema bado kuna wafuasi zaidi wa Mackenzie wanaopiga kambi katika msitu wa Shakahola.
Licha ya kukamatwa kwake na kuendelea kuzuiliwa, polisi hivi majuzi wamefukua miili mipya iliyozikwa.
Yeye na washtakiwa wenzake watafikishwa tena mahakamani katikati mwa Septemba.
Afisa mkuu wa polisi hata hivyo anasema bado wanahitaji muda zaidi kukusanya ushahidi kabla ya kesi kuanza.