Mgombea wa Kiti cha Urais Nchini Kenya kupitia Chama cha Agano, Waihiga Mwaure amekubali kushindwa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa nchi hiyo, baada ya kufuatilia mwenendo mzima wa uchaguzi tangu matokeo yalipoanza kutolewa.
Akizungumza na vyombo vya Habari jijini Nairobi, Waihiga amesema Chama chake cha Agano kimekubali kuwa kimeshindwa na kuitaka tume ya uchaguzi ya IEBC kutangaza matokeo na kuondoa sintofahamu inayoendelea nchini humo kwani vyombo vingi vya Habari vimekuwa vikimuonesha nani akiongoza.
Amesema, “Tumekubali sisi wana Agano tumeshindwa uchaguzi huu, lakini tunaiomba tume ya IEBC kusimama imara na kutokubali kuingiliwa katika utoaji wa matokeo ya uchaguzi na pia imtangaze mshindi maana inajulikana nani ameshinda kwa takwimu za vyombo vya Habari.”
Wakati huo huo, John Sakaja ameibuka mshindi wa wadhfa wa ugavana wa mji mkuu wa Kenya Nairobi, akimshinda mgombea wa Jubilee kutoka Muungano wa Azimio Polycarp Igathe baada ya kupatia kura 699,392 dhidi ya Igathe aliyepatia kura 573, 516.
Chama cha ODM, kupitia kwa mgombea wake, Edwin Sifuna kimepatia kura 716,876 na IEBC kumudhinishwa kuwa Seneta wa jiji la Nairobi baada ya kumshinda mgombea wa UDA Margeret Wanjiru aliyepata kura 524,091.