Kenya imetuma kikosi maalum cha polisi kudhibiti mapigano ya kijamii yanayozidi kuongezeka katika mji wa Sondu, Magharibi mwa mpaka wa Kericho-Kisumu.
Watu saba wamefariki na wengine kadhaa wakiripotiwa kuyahama makazi yao kutokana na kuzuka kwa makabiliano mapya yaliyoanza siku ya Jumatano.
Katika taarifa yake, Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya, Kithure Kindiki alisema wakuu wa usalama wa mashinani kutoka kaunti zote mbili za Kisumu na Kericho watahamishwa kufuatia makabiliano hayo.
"Watu wamefariki, mali kuharibiwa na hali ya raia imedhoofishwa sana katika siku mbili zilizopita," alisema waziri Kindiki .
Viongozi wa eneo hilo wametaka kutatuliwa kwa haraka kwa mzozo wa mpaka kati ya jamii zinazozozana.
Watu watatu waliuawa katika mashambulio kama hayo mwezi Julai.
Mji wa Sondu una historia ya ghasia mbaya za kikabila wakati wa uchaguzi, uhasama huo ukihusishwa na siasa na mivutano mingine ya kijamii.