Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kenya: Jaji Mkuu David Maraga Amwambia Rais Kenyatta Kuwa Hana Mamlaka ya Kuingilia Uhuru wa Mahakama

JAJI MKUU Kenya: Jaji Mkuu David Amwambia Rais Kenyatta Kuwa Hana Mamlaka ya Kuingilia Uhuru wa Mahakama

Fri, 5 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahusiano kati ya muhimili wa Mahakama na Serikali huko nchini Kenya yanaweza kuingia shubiri kwa mara nyingine baada ya Jaji Mkuu wa taifa hilo kumwambia Rais kuwa muhimili wa Mahakama hauwezi kupokea amri kutoka muhimili wa serikali.

Jaji Mkuu, David Maraga amesema kuwa Amri ya Serikali namba 1 ya 2020 iliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta haiwezi kugusa muhimili wa Mahakama na wala Kamisheni ya Huduma za Mahakama ya nchi hiyo kwakuwa taasisi hizo zote zipo huru dhidi ya serikali.

Amri hiyo ya Serikali iliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatano na ikionesha kusainiwa Mei 11, 2020 ilipewa jina ‘’The Organisation of Government and Regularises Changes in Government’’.

Siku ya Alhamisi, Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga alitoa taarifa kwa vyombo vya Habari na Umma kuhusiana na amri hiyo, ambayo inampa mamlaka Rais kuagiza na kuratibu shughuli za wizara na idara za serikali.

‘’Amri hiyo haiwezi kubadilisha au kutenga shughuli kwenye mihimili mingine yenye hadhi sawa na serikali, au hata taasisi nyingine huru na tume huru’’, Maraga alisema katika taarifa yake.

Vilevile, Jaji Maraga anasema kuwa Mahakama si Wizara au Idara ya serikali, kwahiyo haiwezi kupokea amri za kiserikali au za Rais. Anaongeza kwa kusema kwamba amri hiyo haiwezi kubadilisha lolote katika Mahakama na kuwa amri hiyo itatumika tu, na inaweza kutumika tu kwenye muhimili wa serikali wa taifa hilo.

Vilevile, Jaji Mkuu David Maraga ametaka Ofisi ya Rais Kenyatta kutoa masahihisho mara moja katika kile alichokiita ‘’kosa lisiloweza kukubalika’’.

Hii si mara ya kwanza kwa Muhimili wa Mahakama kuingia katika sintofahamu na Muhimili wa Serikali wa Taifa hilo. Katika hukumu ya kihistoria na kwa mara ya kwanza barani Afrika, mwaka 2017 Mahakama Kuu ya Kenya iliufuta uchaguzi uliompa Rais Kenyatta ushindi wa asilimia 54 kutokana na matatizo yaliyobainika katika upigaji na uhesabuji kura wakati wa Uchaguzi na kutaka serikali kuitisha uchaguzi mwingine ndani ya siku 60, katika kesi iliyowasilishwa mahakamani na aliyekuwa hasimu mkuu wa Kenyatta, Raila Odinga.

Ingawa Rais Kenyatta alikubali na kusema anaheshimu uamuzi huo wa Mahakama Kuu na kuwataka wakenya nao wakubali kwa amani, lakini pia alionesha kukasirishwa na maamuzi hayo ya mahakama na hata kuwaita majaji waliofikia uamuzi huo 'wakora'.

''Mamilioni ya Wakenya walipanga foleni, wakafanya uamuzi wao, ila watu sita tu (majaji) wamekaa na kuamua kwenda kinyume na matakwa ya watu'', alisema Kenyatta kwa hasira.

Hata hivyo, hatua hii ya mahakama inatakwa kama kiashirio cha kukua kwa demokrasia na uhuru wa mihimili ya dola katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live