Macho na masikio ya watu wengi duniani kwa sasa, yapo nchini Morocco ambapo oparesheni kubwa ya kumuokoa mtoto Rayan mwenye umri wa miaka mitano, aliyetumbukia kwenye kisima chembamba chenye urefu wa futi 100 (mita 32), inaendelea huku vikosi vya uokoaji vikiwa kwenye hatua za mwisho ya kumuokoa mtoto huyo baada ya kukaa ndani ya kisima hicho kwa siku tano.
Rayan alitumbukia kisimani Jumanne ya Februari Mosi, majira ya jioni wakati baba yake akiwa anakifanyia matengenezo kisima hicho kilichopo katika Kijiji cha Ighran kilichopo katika Jimbo la Chefchaouen nchini Morocco ambapo mtoto huyo aliteleza na kutumbukia ambapo juhudi za kumtoa akiwa salama zilikawa kutokana na wembamba wa kisima hicho.
Haukupita muda mrefu, habari za kutumbukia kwake kisimani zilianza ku-trend kwenye mitandao ya kijamii na kugusa hisia za wengi, ambapo vikosi vya uokoaji vya nchi hiyo, vilielekea eneo la tukio haraka na kuanza kuangalia namna ya kumuokoa akiwa hai.
Hata hivyo, juhudi hizo zimekumbana na kizingiti kikubwa kutokana na wembamba wa kisima hicho lakini pia kiasili, ardhi ya eneo hilo ni ya mchanga uliochanganyikana na miamba, hivyo umakini mkubwa unatakiwa ili kuzuia asije akabomokewa na kufukiwa na kifusi.
Ni hapo ndipo mpango maalum wa kumuokoa ulipoanza kufanyiwa kazi, ambapo vikosi vya uokoaji vimelazimika kuchimba shimbo kubwa pembeni ya kisima hicho, kisha kuanza kuchimba chini kwa chini kuelekea ndani ya kisima hicho.
Magreda zaidi ya matano yalielekea eneo la tukio na kuanza kazi hiyo, huku helikopta maalum ikionekana kando ya eneo la tukio, kwa ajili ya kumkimbiza hospitali mtoto huyo mara atakapotolewa salama.
Hata hivyo, kazi haikuwa nyepesi, kwa muda wa siku tano mfululizo, vikosi vya uokoaji vimeendelea kupambana kufa na kupona kuhakikisha mtoto huyo anaokolewa salama, ambapo vikosi hivyo vililazimika kuingiza mtungi wa hewa ya oksijeni na bomba la maji kwa ajili ya kuendelea kumfanya mtoto huyo abakie kuwa hai wakati juhudi za kumuokoa zikiendelea.
Picha kutoka chini ya kisima hicho, zimemuonesha mtoto huyo akiwa hai ingawa anaonekana kuwa na majeraha kadhaa usoni na damu zilizoganda kwenye paji lake la uso.
Wakati hayo yakiendelea, mamia ya wananchio wa Morocco wamejazana eneo la tukio, wengine wakilala na kushinda hapo kusubiri mtoto huyo aokolewe, huku vyombo vingi vya habari vikiripoti moja kwa moja kutoka eneo la tukio, hali iliyozidi kugusa hisia za wengi wanaofuatilia moja kwa moja maendeleo ya tukio hilo.
Katika mtandao wa twitter, wafuatiliaji kutoka sehemu mbalimbali duniani, wameendelea kumuombea mtoto huyo kwa Mungu ili atoke salama, chini ya hashtag ya #SaveRayan ambayo imeendelea kutrend kwa kasi kubwa kwa siku zote ambazo mtoto huyo amenasa kisimani.
Habari mpya za Jumamosi asubuhi, Februari 5, 2022 ni kwamba waokoaji wamebakiza mita nne pekee kumfikia mtoto huyo na kwamba jitihada zinaendelea kwa kasi na umakini mkubwa!
Wazazi wa mtoto huyo ni miongoni mwa watu ambao hawajapata hata lepe la usingizi tangu tukio hilo litokee na sasa dua zote zinaelekezwa kwao na kwa mtoto wao ili hatimaye atoke salama na kuungana na wazazi wake.
Endelea kufuatilia Global TV kwa taarifa zaidi kuhusu tukio hili.