Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katumbi ataka uchaguzi wa DRC utenguliwe

Moses Katumbi.jpeg Katumbi ataka uchaguzi wa DRC utenguliwe

Sun, 24 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wagombea watano wa upinzani katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akiwemo Moise Katumbi wametoa mwito wa kufutiliwa mbali uchaguzi huo, wakidai kuwa zoezi hilo la kidemokrasia limekumbwa na wizi wa kura na uchakachuaji wa matokeo.

Viongozi hao wa upinzani wamesema uchaguzi huo hauna itibari ya kisheria kwa kuwa umegubikwa na udanganyifu mkubwa, na hivyo wametoa mwito kwa wafuasi wao kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maandamano ya kupinga matokeo hayo.

Wagombea hao wa urais wa upinzani akiwemo Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Denis Mukwege wamesema katika barua yao kwa Gavana wa Kinshasa kuwa, wataandamana siku ya Jumatano katika mji huo mkuu wa DRC kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Juzi Ijumaa, Tume Huru ya Uchaguzi nchni humo CENI ilianza kutangaza matokeo ya uchaguzi huo uliogubikwa na machafuko, huku baadhi ya waangalizi wa kimataifa wakidai kuwa kumekuwa na dosari nyingi katika mchakazo mzima wa upigaji kura.

Kwa mujibu wa matokeo ya upigaji kura wa Wakongo wanaoishi Afrika Kusini, Marekani, Canada, Ubelgiji na Ufaransa, Rais Felix Tshisekedi anaongoza kwa kura nyingi zaidi ya wapinzani wake. Wagombea wakuu wa urais DRC

Wapiga kura milioni 44 walijiandikisha kupiga kura kuwachagua viongozi wao, ambapo wagombea wa nafasi ya urais ni 20 akiwemo Rais Tshisekedi anayesaka awamu ya pili. Wakongomani pia walipiga kura Jumatano iliyopita kuwachagua wabunge wa kitaifa na wa mikoa, na madiwani wa serikali za mitaa.

Uchaguzi wa Tshisekedi kama rais mwaka 2018 ulikumbwa na shutuma za wizi wa kura na udanganyifu. Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban watu 34 waliuawa na wengine 59 kujeruhiwa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi iliyotangazwa na CENI, matokeo kamili ya uchaguzi huo yatatangazwa kufikia tarehe 31 mwezi huu wa Disemba na Rais mteule anatazamiwa kuapishwa tarehe 24 mwezi Januari 2024.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live