Jumamosi, Kanisa Katoliki, dayosisi ya Nyeri nchini Kenya ilishuhudia historia ikiandikwa baada ya shemasi mmoja ambaye ni kipofu kutawazwa kama kasisi.
Kutawazwa kwake Michael Mithamo King’ori kuliandikisha historia kuwa kasisi wa kwanza kuhudumia kanisa na kondoo wa Mungu akiwa kipofu.
Ibada ya shukurani na kutawazwa kwake iliongozwa na askofu aiyesherehekea na Wakenya wengi kutokana na matendo yake ya busara, Anthony Muheria na kituo cha habari cha kanisa katoliki kilisema kuwa kasisi huyo mpya kipofu ni hadithi ya kipekee ambayo itasimuliwa bila kuchoka kwa vizazi vingi vijavyo.
“Shangwe na shukrani kwa Mungu huku Kanisa Katoliki nchini Kenya likishuhudia kutawazwa kwa njia isiyo ya kawaida kwa kasisi wa kwanza kipofu, Kasisi Deakoni Michael Mithamo King'ori wa Jimbo Kuu Katoliki la Nyeri kuwa kasisi. Hadithi yake ni ya "kwa Mungu, mambo yote yanawezekana."” Sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.
Wengine waliowekwa wakfu sambamba na Mithamo ni; Alexander Murage Wanjiku, Joseph Waihenya Kirira, George Gitonga Wamuyu, Mathew Karimi Njogu na John Wanjohi Nyawira. Kutawazwa kwao kunajiri baada ya Maria Carola kutawazwa kuwa mtakatifu mnamo Jumamosi, Novemba 5, katika hafla iliyoandaliwa katika uwanja wa Kinoru kaunti ya Meru.
Tangazo la kutangazwa kuwa mwenye heri liliidhinishwa na Papa Francis mnamo Desemba 2021 na baadaye kutangazwa na Masista wa Mtakatifu Joseph Cottelengo baada ya muujiza uliohusishwa naye kutambuliwa.