Mamlaka nchini Afrika Kusini zinasema zimearifiwa kuhusu vifo vya washukiwa 31 wa wachimbaji migodi haramu, wanaoaminika kutoka Lesotho, katika mgodi ambao haujatumika huko Free State
Idara ya rasilimali za madini ya Afrika Kusini ilisema katika taarifa kwamba iliarifiwa na serikali ya Lesotho kuhusu vifo hivyo, tarehe 18 Mei, katika shimo la uingizaji hewa la mgodi.
Mgodi huo wa Welkom, Free State, ulifanya kazi mara ya mwisho katika miaka ya 1990, ilisema.
Idara ya rasilimali ya madini ya Afrika Kusini inasema pia imefahamishwa kuwa miili mitatu imetolewa kutoka kwa mgodi huo na wachimbaji haramu wengine.
Inasema kuwa inafanya “kadiri iwezavyo” kufanyia kazi taarifa hii na imekuwa ikishirikiana na wadau wote husika, wakiwemo wamiliki wa awali wa mgodi huo, ili kupata miili hiyo.
Hata hivyo inasema wakaguzi wametathmini tukio hilo na kuamua kuwa hali ka sasa ni hatari sana kupeleka watu huko.
"Viwango vya methane katika shimoni namba 5 ya kuingiza hewa ni ya juu sana. Ni hatari sana kutuma timu ya upekuzi kwenye mgodi huo," idara ilisema.
Matukio ya vifo kwenye migodi ya zamani si ya kawaida nchini Afrika Kusini, huku wachimbaji haramu wakiwemo wahamiaji mara nyingi wakihatarisha afya na usalama wao katika migodi iliyotelekezwa.