Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni binafsi zawekewa mashari chanjo ya corona

91911eaaf0bf1bb0fa5ea7c8441fb8c4 Kampuni binafsi zawekewa mashari chanjo ya corona

Tue, 13 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI ya Uganda imeondoa vizuizi kwa kampuni binafsi kuingiza chanjo ya ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, lakini imeweka masharti magumu ambayo lazima yatimizwe.

Chama cha Madaktari Uganda kimesema kuruhusiwa kwa kampuni binafsi kuingiza na kutoa chanjo hizo kutaboresha upatikanaji wake na kusaidia serikali kukabiliana na utoaji huduma kwa wagonjwa na kupunguza vifo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Afya, Dk Jane Aceng alisema wamekuwa wakipokea maombi mengi kutoka mashirika binafsi ambayo yanataka kuagiza chanjo hiyo.

Alisema kutokana na maombi kuwa mengi, wameona ni lazima yawekwe masharti ambayo yakitimizwa kampuni husika itaruhusiwa kuingiza chanjo hiyo nchini.

Dk Aceng alisema miongoni mwa masharti hayo ni chanjo inayoingizwa lazima iwe imeidhinishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kwa matumizi ya dharura na kupitishwa na Mamlaka ya Dawa ya Taifa (NDA) kutumika nchini.

Alisema pia kampuni inapaswa kubainisha chanjo ilipotengenezwa na itaingizwa kutoka nchi gani na jinsi itakavyohakikisha inahifadhiwa vizuri bila kuharibika.

Naye Waziri wa Nchi Anayesimamia Afya kwa Wote, Robinah Nabbanja alisema ingawa kampuni binafsi zinataka kuleta chanjo hiyo, lakini uwezo wa kuzipata ni mdogo kutokana na kuwapo mahitaji makubwa duniani.

“Kampuni nyingi za binafsi zinataka kuagiza chanjo hizo, lakini hofu yetu ni ubora wa chanjo watakazoagiza. Watu wengine wanaweza kuagiza chanjo zisizo na kiwango, kama serikali tu haipati chanjo wenyewe watapata wapi?” alihoji.

Chanzo: www.habarileo.co.tz