Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni 3 za ndege Kenya zazuiwa kuingia nchini

1590f80c16bdcf38f84b13f0d0f48738 Kampuni 3 za ndege Kenya zazuiwa kuingia nchini

Fri, 28 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imezuia kampuni tatu za ndege za Kenya kuingia nchini.

Zimezuiwa mpaka hapo nchi hiyo, itakaporuhusu ndege za Tanzania kutua nchini humo bila ulazima wa abiria wote kukaa karantini siku 14 kwa kisingizio cha kudhibiti ugonjwa wa Covid-19.

Hatua hiyo inatokana na Kenya juzi kutangaza orodha ya ruhusa ya nchi nyingine 130 kuingia nchini humo bila masharti ya kukaa karantini siku 14. Tanzania haipo orodha hiyo, hatua inayolazimu abiria na raia wa Tanzania kukaa karantini hiyo wanapoingia Kenya.

Kwa mara ya kwanza Julai 31 mwaka huu, TCAA ilitangaza kuzuia ndege za Kenya Airways (KQ) kuingia nchini baada ya Serikali ya Kenya siku hiyo hiyo kutangaza orodha ya nchi 19, ambazo raia wake wanaruhusiwa kuingia nchini humo bila karantini na Tanzania haikuwepo.

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari aliiambia HabariLEO jana kuwa zuio hilo ni la kweli na kuzitaja kampuni zilizozuiwa kuwa ni Air Kenya, Safari Link Aviation na Fly540, zote za jijini Nairobi. Alisema Fly540 ilishaandika barua ya kutaka kuanza safari zake nchini wiki ijayo.

"Ni kweli, mwanzo tulizuia ndege za KQ kuja baada ya wao kufungua anga kwa nchi zote kuingia kwao isipokuwa Tanzania. Walisema kwamba kila baada ya muda watatoa orodha ya nchi watakazozifungulia anga, tukawa na matumaini kwamba hili litakwisha.

"Juzi (Jumanne) wametangaza nchi nyingine 130 zaidi kuzifungulia anga kuingia Kenya bila masharti ya karantini na Tanzania haipo. Ndege za Tanzania kama Air Tanzania au Precision ikitua Kenya lazima abiria wake wote wakae siku 14 karantini,"alisema Johari.

Alisema awali kabla ya zuio hilo, ndege za Kenya zingeweza kutua nchini bila ulazima wa kuwekwa karantini abiria wote na wangesafirisha abiria kwenda Kenya bila kuwekwa karantini nchini mwao, lakini ndege za Tanzania zikitua Kenya, lazima karantini.

Johari alisema mara kadhaa Serikali ya Kenya imekuwa ikisema bila maandishi kwamba haijaifungia Tanzania anga, lakini kuweka lazima ya kukaa karantini huku nchi nyingine zikiruhusiwa bila karantini ni sawa na kuzuia.

"Ni mfanyabiashara au mtalii gani atakubali kwenda kuwekwa karantini siku 14 Kenya wakati ndipo aingie mjini kufanya utalii au shughuli zake, hii ni sawa na kuzuia wasiende," alisema.

Mkurugenzi huyo alisema wataondoa katazo hilo, pale ambapo Kenya kwa maandishi itaiweka na kuitangaza Tanzania kwenye orodha ya nchi zinazoweza kusafirisha abiria bila masharti ya karantini, kama nchi nyingine duniani zikiwamo za Afrika Mashariki.

"Wenzetu wamekuwa wakizungumza kwa maneno, sisi tunazungumza kwa maandishi. Haiwezekani wao ndege zao zikibeba abiria hapa, ziruhusiwe kutua kwao bila lazima ya karantini, lakini ikishakua Air Tanzania au Precision, basi lazima karantini, hii haijakaa sawa,"alisema Johari.

Johari alisema Kampuni ya Fly540 iliandika barua hivi karibuni kuwa itaanza safari zake nchini wiki ijayo. Alisema kwamba kutokana na katazo hilo, haiwezi tena kuja mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.

Ndege za kampuni hizo zilizozuiwa, kwa kawaida husafirisha watalii kila siku kuelekea mkoani Kilimanjaro kwenye Mlima mrefu Afrika na visiwani Zanzibar.

Kampuni ya Kenya Airways iliwekewa zuio la kuingia Tanzania baada Serikali ya Kenya mwishoni wa Julai kuiondoa Tanzania katika orodha ya nchi 19, ambazo raia wake hawatalazimika kuwekwa karantini kwa siku 14 watakapoingia nchini humo.

"Kinachoshangaza zaidi ni kwamba mataifa ambayo maambukizi ya virusi vya corona yapo juu sana, yameruhusiwa kutua Kenya na abiria wanaingia mjini popote bila karantini, lakini Watanzania, lazima karantini," alisema.

Alisisitiza kuwa zuio kwa ndege za kampuni hizo tatu ni kuanzia Agosti 25 mwaka huu na litaendelea mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo. Alifafanua kwamba hawalazimiki kuomba leseni upya, kwa kuwa leseni zao zipo, ila kilichozuiwa ni kutua nchini.

Tanzania ilitangaza kufungua anga lake kwa ndege kutoka taifa lolote Mei 18 mwaka huu, baada ya juhudi kubwa za serikali kudhibiti kasi ya maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha Covid-19.

Baada ya kufungua anga hilo, ndege za mashirika mbalimbali zilianza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo Dar es Salaam na Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wa Zanzibar.

Ndege zinazotua kuanzia Juni mwaka huu ni za Ethiopia Airlines, Qatar, KLM, Turkish Airlines, Emirates na nyingine nyingi.

Chanzo: habarileo.co.tz