RAIS wa Rwanda, Paul Kagame anatarajiwa kuitembelea Malawi katika ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia Agosti 11 mwaka huu. Ziara hiyo itakuwa ya kwanza tangu Rais Mpya Lazarus Chakwera aingie madarakani.
Katika ziara hiyo, Kagame anatarajiwa kuwa na mazungumzo na kiongozi huyo wa Malawi ambapo mikataba ya kibiashara inatarajiwa kusainiwa kati ya mataifa hayo mawili pamoja na kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Mara ya mwisho kiongozi huyo wa Rwanda kuitembelea Malawi ilikuwa wakati wa Hayati Rais Bingu wa Mutharika ambapo alihudhuria hafla ya kufunguliwa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 3.3 iliyopewa jina la Kagame.
Kwa mujibu wa Rais Chakwera, Kagame ni mfano wake mzuri katika kujenga jamii yenye umoja na mshikamano kama alivyofanya nchini kwake Rwanda ambapo aliwatoa katika shida ya mauaji ya kimbari na ukabila na kuifanya Rwanda kuwa taifa moja.