Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata Katibu Mkuu mpya

1b9d302d3d65fb3f02bf818c1962cc14.png Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata Katibu Mkuu mpya

Tue, 23 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JUMUIYA ya Afrika Mashariki wiki hii inatarajia kuingia kwenye awamu mpya ya uongozi kwa kupata Katibu Mkuu mpya kutoka nchini Kenya.

Hatua hiyo imekuja baada ya Katibu Mkuu anayeshika nafasi hiyo kwa sasa kutoka nchini Burundi, Balozi Liberat Mfumukeko kumaliza kipindi chake cha miaka mitano ya uongozi.

Wakati hayo yakiendelea, vikao muhimu vya jumuiya hiyo vitaendelea wiki hii kwa kuanza na ngazi ya maofisa waandamizi, makatibu wakuu, mawaziri kabla ya marais wanaotarajia kukutana Jumamosi ya Februari 27.

Ofisa Uhusiano wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Florian Mutabazi amethibitisha Balozi Mfumukeko kumaliza muda wake na kueleza kuwa, nafasi hiyo inapatikana kwa nchi wanachama kuachiana na kwamba tayari nchi za Uganda, Rwanda, Tanzania na Burundi inayoshikilia nafasi hiyo zimetoa makatibu wakuu na sasa ni zamu ya Kenya.

“Kenya wakati inashikilia nafasi ya uongozi wa jumuiya hakukuwa na cheo cha Katibu Mkuu, hivyo kwa sasa atapatikana kutoka nchini humo ambapo itapendekeza jina kisha kujadiliwa na vikao jumuiya,” alisema Mutabazi.

Alisema katika vikao vinavyoendelea jina hilo litawasilishwa kujadiliwa kisha kupelekwa katika kikao cha marais ili kupitishwa na aliyepitishwa atakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano pekee bila kurudia.

Alisema Balozi Mfumukeko anamaliza muda wake mwishoni mwa wiki hii, lakini ataondoka madarakani Aprili baada ya kukamilisha makabidhiano na masuala mengine.

Akizungumzia mkutano wa wakuu wa nchi za Jumiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika Jumamosi ijayo, Mutabazi alisema bado nchi wanachama hazijathibitisha kushiriki, lakini mchakato unaendelea wiki hii katika vikao vya awali.

Mfumukeko aliteuliwa wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC wa Februari, 2016 kuchukua nafasi ya Dk Richard Sezibera wa Rwanda na alianza kufanyakazi Aprili 26, 2016.

Akizungumza na Gazeti la The East African, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC, Profesa Manase Nshuti ambaye ni Waziri wa Nchi wa Rwanda anayeshughulikia masuala ya EAC alikataa kutoa maoni juu ya utawala wa Mfumukeko.

"Kuna mambo mengi pamoja na uhusiano na vyombo vingine vya EAC ambavyo vingeweza kufanywa vizuri. Lakini sitatoa maoni mengi kwa sababu maoni yangu yanaweza kutolewa nje ya muktadha,” alisema Prof Nshuti.

Inadaiwa kuwa, wakati akishikilia nafasi hiyo, Balozi Mfumukeko nchi yake ya Burundi haijatoa zaidi ya dola za Marekani milioni 12, huku Sudan Kusini ikidaiwa dola milio ni 27.

“Jukumu la Katibu Mkuu ni kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili na nchi washirika na kuhakikisha kuwa kuna fedha kwa shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Denis Namara.

“Alishindwa kuhakikisha nchi yake Burundi na Sudan Kusini zinatoa michango yao kwa wakati. Nina shaka hata kama aliwahi kukanyaga Sudan Kusini kuwashawishi walipe,” alisema Namara.

Hata hivyo, Balozi Mfumukeko amepinga lawama hizo na kusema alihamasisha mipango ya uhamasishaji katika upatikanaji fedha kwa kushirikiana na vyombo vikuu vya jumuiya.

Chanzo: habarileo.co.tz