Serikali ya Ufaransa inajaribu kuonyesha kuwa uhusiano wake na Morocco ni wa kawaida kwa kufanya jitihada za kukana kuwa, Rabat imekataa msaada wa Paris kwa wathirika wa tetemeko la ardhi katika nchi hiyo ya Kiafrika.
Catherine Colonna, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa, amejaribu kukomesha utata uliopo kuhusu uhusiano mbaya kati ya nchi hizo mbili. Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amedai kuwa, Morocco haijakataa msaada au pendekezo lolote la Paris. Colonna aliendeleza matamshi yake ya kuingilia kati akisema: Morocco inaweza kuainisha mahitaji yake na kasi ya kupokea misaada. Catherine Colonna
Jumamosi iliyopita tetemeko la ardhi la takriban 7 kwa kipimo cha Richter lilitokea katika maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika na kusababisha uharibifu mkubwa.
Ripoti zinasema viongozi wa Rabat wamekataa mapendekezo ya Ufaransa ya kutuma misaada kwa wathirika wa janga hilo la kimaumbile licha ya msisisitizo wa mashirika ya serikali na jumuiya za kiraia za Ufaransa wa kutaka kushirikishwa katika operesheni za kutoa misaada nchini humo. Hadi sasa Morocco imepokea misaada kutoka nchi kama Uhispania, Uingereza, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Huku akithibitisha habari hiyo, Arnaud Fraisse, mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Ufaransa, la Waokoaji Wasio na Mipaka (Secouristes Sans Frontières) ametangaza kuwa Morocco inazuia kuingia nchini humo timu za misaada za Paris wa ajili ya kuwasaidia walioaridhiwa wa tetemeko la ardhi.
Serikali ya Morocco imekataa msaada wa Ufaransa huku baadhi ripoti za vyombo vya habari zikisema kuwa, Mfalme Mohammed VI wa Morocco amekataa kupokea simu ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron. Wataalamu na wanahistoria wanasema kuwa uhusiano kati ya Ufaransa na Morocco haujawahi kuharibika kwa kiwango cha sasa.
Pierre Vermeren, mwanahistoria na profesa katika Chuo Kikuu cha Sorbonne, anaamini kwamba hatua hiyo ya Mfalme wa Morocco ya kukataa kujibu sumu ya Rais Emmanuel Macron ni ishara ya wazi ya kisiasa ya kuharibika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Morocco inaonekana kujiunga na nchi kadhaa za Afrika ambazo zimeamua kukata au kupunguza kwa kiwango kikubwa uhusiano wao na mkoloni huyo wa amani, yaani Ufaransa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.